DODOMA-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameagana na aliyekuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa katika Ofisi ya Waziri wa Fedha, Treasury Square jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine, alimpongeza Dkt. Chuwa kwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake mengine baada ya kustaafu, Dkt. Chuwa kwa upande wake alimshukuru Mhe. Dkt. Nchemba, kwa miongozo na usimamizi mahiri wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, hatua iliyoifanya Taasisi hiyo kuwa moja ya Taasisi inayoheshimika duniani.

Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alimteua Dkt. Amina Msengwa, kuchukua nafasi ya Dkt. Albina Chuwa, ambaye amestaafu rasmi baada ya kuongezewa vipindi viwili vya mikataba baada ya kustaafu miaka michache iliyopita kutokana na umahiri wake katika kusimamia masuala ya takwimu nchini ikiwemo Sensa za Watu na Makazi zilizofanyika chini ya usimamizi wake.