Dkt.Nchemba amuaga Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia

DAR-Waziri wa Fedha. Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameagana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda Afrika Mashariki na Kusini, Bi. Victoria Kwakwa, anayekaribia kumaliza muda wake, wakati wa Chakula cha Jioni alichomwandalia jijini Dar es Salaam, na kumshukuru kwa jitihada zake za kusimamia maslahi ya Tanzania kwa upendo wa hali ya juu katika kipindi chote alichoitumikia Taasisi hiyo kubwa ya Fedha Duniani.
Kwa upande wake, Bi. Victoria Kwakwa, alisifu ushirikiano alioupata kutoka kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, na kwamba anajivunia mafanikio makubwa ambayo Tanzania imeyafikia katika nyanja za kiuchumi na kijamii, kwa kuwa na uchumi imara, ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika.
Alisema kuwa, anastaafu kazi lakini ana uhakika Makamu Mpya wa Rais wa Benki ya Dunia atakayechukua nafasi yake (Jina linahifadhiwa) kuzisimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, atatoa ushirikiano mkubwa kwa Tanzania ili nchi iweze kufikia malengo iliyokusudiwa kupitia Benki ya Dunia.
Tukio hilo la kumuaga Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Bi. Victoria Kwakwa, imehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi John Ulanga, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete, Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, na Maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Benki ya Dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news