MOROGORO-Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2025.
Doyo ametangaza nia ya kuwani nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Machi 14,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari Mkoa wa Morogoro.
Ameeleza kuwa, Tanzania ni nchi ya kidemokrasia ambapo kila Mtanzania mwenye sifa anayo haki ya kuchagua au kuchaguliwa.
Pia,aliongeza kuwa, yeye mwenyewe ana sifa zote za kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo umri usiopungua miaka 45, umri ambao tayari amevuka, na afya ya kuhimili majukumu ya urais an
Akizungumza kuhusu umuhimu wa uchaguzi huu, Doyo alisema kuwa uchaguzi huu ni wa sita tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, na hivyo ni uchaguzi muhimu sana kwa taifa letu.
Alisisitiza kuwa, kama Mtanzania mwenye haki ya kikatiba, amejitathmini kifikra, kiuwezo, na kiuweledi, na kujiridhisha kuwa ana uwezo wa kumudu nafasi hiyo.
Aliendelea kusema kuwa, bado kuna masuala mengi muhimu ambayo hayajapata kipaumbele kikubwa katika taifa letu, na hivyo ameamua kugombea nafasi hii ili kutoa mchango wake katika kushughulikia masuala hayo muhimu.
Miongoni mwa hayo ni Ajira, Elimu, Kilimo na Ufugaji, Rasilimali za Maji,Kuziba Mianya ya Ukwepaji wa Kodi na Kupambana na Rushwa,Kujenga Taifa la Walipa Kodi,Kuongeza Jitihada kwa Watoto wa Kike katika Elimu na Teknolojia, Kuimarisha Muungano wetu, Kuimarisha Sekta Binafsi ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli za kiserikali na kijamii na Kuweka nguvu katika Sekta ya Madini.