Finland yaipongeza Tanzania kwa utekelezaji wa miradi

DAR-Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Finland ukiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara inayosimamia Afrika, Mashariki ya Kati na Latin America wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, Bi. Helena Airaksinen, ulioambatana na Balozi wa nchi hiyo hapa nchini, Mhe. Theresa Zitting.
Akizungumza katika mkutano huo, Bi. Omolo alisema kuwa, ujumbe huo umekuja kwa lengo la kufanya tathmini ya kiutendaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo zilizotekelezwa kupitia msaada wa nchi hiyo kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 ili kupanga mikakati mingine kwa mwaka 2024 hadi 2028.

Alisema kuwa tangu mwaka 2010 Finland ilitoa kiasi cha Euro zaidi ya milioni 351 ili kutekeleza miradi mbalimbali ambayo imekamilika kwa takribani asilimia 87 na asilimia 13 ya miradi hiyo bado ipo katika hatua ya utekelezaji.

“Makubaliano ya ushirikiano wa kimaendeleo wa hivi karibuni kati ya nchi hizi mbili ulijikita kutekeleza program za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuimarisha masuala ya uchumi, kuhamasisha kutengeneza ajira, eneo la ubunifu, kujenga uwezo kuhusu kodi na utawala bora katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024”, alisema Bi. Omolo.

Alisema kuwa kutokana na program kumalizika mwaka 2024 ni dhahiri kunahitajika majadiliano yatakayowezesha kuwa na program mpya zinazotakiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2025.

Alisema katika majadiliano hayo Timu za Wataalamu kutoka pande mbili zitaainisha maeneo mapya ya ushirikiano kulingana na Dira ya Taifa ili yaweze kufanyiwa kazi na wadau hao wa maendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara inayosimamia Afrika, Mashariki ya Kati na Latin America wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, Bi. Helena Airaksinen, alisema kuwa maeneo ya ushirikiano kati ya nchi yake na Tanzania yameendelea kuongezeka licha ya kubadilishwa kwa Sera za nchi.

Alisema kuwa zipo nchi nyingi ambazo zimeondolewa katika utekelezaji wa program kupitia nchi yake lakini Tanzania itaendelea kuwa mshirika muhimu katika kuchochea maendeleo ya pande hizo mbili kutoka na juhudi zake katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Majadiliano kati ya pande hizo mbili yalihusisha pia wajumbe kutoka Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Madini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Tume ya Mipango.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news