Hatifungani ya Zanzibar Sukuk kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo

DAR-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefungua dirisha la uwekezaji katika hati fungani inayofuata misingi ya dini ya Kiislamu, Zanzibar Sukuk, ambayo inalenga kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo visiwani humo.
Akizungumza baada ya kikao na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Saada Mkuya, kilichofanyika katika ofisi za Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu, Bw.Emmanuel Tutuba alieleza kuwa kuanzishwa kwa hati fungani ya Sukuk ni matokeo ya utafiti uliofanyika mwaka 2023.

Utafiti huo ulihusisha makundi yaliyo nje ya mfumo rasmi wa kifedha na kubaini kuwa baadhi ya watu, kutokana na imani zao za kidini, walikuwa wakishindwa kushiriki kwenye uwekezaji unaotoa riba.
"Kufuatia utafiti huu, tulifanya marekebisho kwenye Sheria ya Benki Kuu, Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha, pamoja na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ili kuwezesha utekelezaji wa masoko haya ya fedha kwa kuzingatia misingi ya Kiislamu," alisema.

Aliongeza kuwa fursa hii ya uwekezaji inaruhusu wananchi wa ndani na nje ya nchi kushiriki kikamilifu, hivyo kuchochea matumizi ya huduma rasmi za kifedha.

"Ni uwekezaji halali kisheria unaowapa wananchi wote fursa ya kushiriki kulingana na imani zao, hivyo kusaidia miradi ya maendeleo ya serikali, kukuza uchumi, na pia kuwanufaisha wawekezaji," alieleza.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya, alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kupata fedha kupitia hati fungani ya Sukuk kwa ajili ya kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo.

"Miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali ya matibabu ya saratani ya Binguni, ujenzi wa kilomita 40 za barabara visiwani Unguja na Pemba, maboresho ya miundombinu ya umeme, na ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani," alisema Dkt. Mkuya.
Alifafanua kuwa mwitikio kutoka kwa wananchi wa dini zote pamoja na taasisi mbalimbali umekuwa mkubwa, huku serikali ikilenga kukusanya shilingi trilioni 1.115. Katika awamu ya kwanza, lengo ni kukusanya shilingi bilioni 600.

Dirisha la uwekezaji katika hati fungani hiyo, ambayo kiwango cha chini cha uwekezaji ni shilingi milioni moja, lilifunguliwa tarehe 6 Machi 2025 na linatarajiwa kufungwa tarehe 11 Aprili 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news