Heshima hii ya Morocco Square inatokana na upendo wa Rais Dkt.Samia-NHC

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC), Bw. Hamad Abdallah amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuukwamua Mradi wa Morocco Square ambao kwa sasa umeleta heshima kubwa kwa Taifa huku ukichagiza katika kukuza uchumi na pato la taifa.
Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 21,2025 na Elias Msese ambaye ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Milki za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi huyo katika uzinduzi wa awali wa Mradi wa Morocco Square jijini Dar es Salaam.

"Kwanza ninatoa shukurani kwa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kukamilisha mradi wetu wa Morocco Square.

"Kama mtakumbuka ulikuwa umekwama kidogo, lakini sasa hivi umeshakamilika kwa asilimia 100. Leo, tunachokifanya kama shirika ni uzinduzi wa awali, kwa kuwa tayari taratibu zote za kupangisha tulishazikamilisha kwa asilimia 100."

Pia, amesema watu wote walionunua tayari wanaishi katika jengo hilo la Morocco Square.

Msese amekumbushia pia kuwa, kuna hoteli ya kisasa ya King Jada ambayo inaendelea kutoa huduma katika jengo hilo.

"Kwa hiyo, kikubwa ambacho tumekuja leo kwenye tukio hili ni kuwafahamisha Watanzania wote wajue sasa kwamba tayari Morocco Square ipo live na makazi tayari watu wapo na wanaishi hapa."

Lakini, pia amesema maduka mbalimbali zikiwemo ofisi za sekta binafsi na Serikali zinatoa huduma katika jengo hilo.

Amesema, uzinduzi wa leo unalenga kutoa ufahamu na uelewa kwa Watanzania kwamba tayari mradi huo mkubwa nchini unatoa huduma mbalimbali.

Pia, ametoa wito kwa Watanzania kuweza kufika Morocco Square kwa ajili ya kujipatia huduma mbalimbali ikiwemo mavazi na vifaa vya umeme ambavyo vingi vinapatikana kwa bei ya ofa kuelekea msimu wa sikukuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news