DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa huduma jumuishi za kifedha ni kiungo muhimu cha ukuaji wa uchumi, kupunguza umasikini na kuchochea maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Amesema Serikali kwa kutambua hilo imedhamiria kuendelea kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha sekta ya kifedha inazidi kuwa jumuishi, fanisi, na yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.
Amesema hayo leo Machi 3, 2035 alipozindua huduma mpya za kidijitali za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.

“Mpango Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023 - 2028 ni mwendelezo wa mafanikio yaliyopatikana kupitia Mpango Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha uliokamilika Desemba 2022.

“Mkakati huu umeainisha malengo mahsusi ambayo kama nchi tunaazimia kuyatekeleza ili kufikia uchumi wa kidijitali.”
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Sauda Msemo amesema sekta ya fedha imeendelea kuwa na ustahimilivu na hivyo kuwezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kufanyika.
Aidha, Naibu Gavana huyo ametoa wito kwa taasisi zote za kifedha zifuate viwango bora vya usalama wa mitandao na kugundua haraka pale panapotokea udanganyifu wa aina yoyote.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema lengo la uzinduzi wa huduma hizo za NBC kidijitali ni kuboresha utoaji wa huduma za kifedha na kuzifanya zipatikane kwa urahisi.
“Huduma hizo ni pamoja na ufunguaji wa akaunti, kuhamisha fedha, kupata mikopo bila ya kwenda katika tawi.”