NA KANDANA LUCAS
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya amefanya ziara ya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya na baadhi ya Mahakama za Mwanzo ndani ya Kanda ya Musoma ikiwa ni ukaguzi wa robo ya kwanza ya mwaka 2025.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya akisikiliza maelezo kutoka kwa Mhandisi wa ujenzi Allan John wa kampuni ya Sky Ward inayojenga mradi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Mugumu.
Akizungumza na Mahakimu na Watumishi wote wa Mahakama alizotembelea, hivi karibuni Mhe. Mtulya alitoa pongezi kwa utendaji kazi mzuri kisha alisisitza kuhusu usikilizaji wa mashauri kwa wakati ili kuepuka kumaliza mwaka na mashauri mengi au kuzalisha mlundikano wa mashauri.
“Sisi viongozi kupitia vikao vyetu vya Menejimenti vya Kanda, tuna mkakati maalumu wa kuhakikisha kila mwaka hatuvuki na mashauri ya mlundikano. Kwa mwaka huu tunatarajia kuanza mapema uchambuzi wa mashauri yote yanayokaribia kuwa mlundikano ifikapo mwezi Juni 2025 (nusu mwaka), ili yaweze kupewa kipaumbele cha kusikilizwa na kutolewa maamuzi mapema na hivyo tutaepuka kutumia nguvu kubwa tunapoelekea kufunga mwaka 2025,” Jaji Mtulya alisema.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Serengeti (hawapo pichani) katika ukaguzi alioufanya hivi karibuni.

Mhe. Mtulya pia aliwakumbusha na kuwahimiza watumishi wote kuhusu masuala mengine kama vile Mahakama zote za Mwanzo zinazosajili mashauri chini ya 260 kwa mwaka, kuhakikisha zinavuka mwaka bila mashauri yaani (zero case), kuhakikisha mashauri yenye mahabusu wa makosa madogo madogo katika Mahakama za Mwanzo yanaamuliwa kwa haraka ili kuepuka msongamano magerezani, kusikiliza kwa wakati mashauri ya talaka, ndoa na mirathi pamoja na kuimarisha ulinzi wa mipaka ya maeneo ya Mahakama kwa kuweka alama tambuzi (bikoni).
Aidha katika ukaguzi huo, Jaji Mtulya alitembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Mugumu ambapo alipongeza hatua iliyofikiwa na kutoa rai kwa Mkandarasi kukamilisha mradi huo, kwa kuzingatia muda uliopangwa ili kuiwezesha Mahakama hiyo kuwa na jengo lake kwani kwa sasa inatumia majengo ya Halmashauri ya Wilaya Serengeti.
Viongozi wengine walioambatana na Jaji Mtulya katika ukaguzi ulioanza tarehe 3 Machi.2025 hadi tarehe 6 Machi.2025, ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Mhe. Salome Mshasha na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Bw. Leonard Maufi, ambao kwa nyakati tofauti walipongeza utendaji kazi wa watumishi wote katika Mahakama zilizotembelewa licha ya uchache wao na kuahidi kushughulikia changamoto mbalimbali zilizoibuliwa na watumishi katika ukaguzi huo.
Mradi wa ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Mugumu-Serengeti ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Aprili 2025.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Salome Mshasha akifafanua jambo wakati wa ukaguzi huo.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Bw. Leonard Maufi akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutawala na utumishi kwa watumishi wa Mahakama ya Wilaya Tarime (hawapo pichani).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine, wakiwemo watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Ikizu-Bunda baada ya ukaguzi.
Viongozi mbalimbali wa Mahakama na Taasisi nyingine (Wadau wa Mahakama) wakiwa pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya, (katikati mstari wa mbele) baada ya ukaguzi wa Gereza la Mahabusu na Wafungwa Wilaya ya Musoma.
Idadi ya Mahakama zilizokaguliwa na viongozi hao ni 15 ambazo ni Mahakama ya Mwanzo Kukirango-Butiama, Mahakama ya Wilaya Butiama, Mahakama ya Wilaya Bunda, Mahakama ya Mwanzo Ikizu-Bunda, Mahakama ya Mwanzo Mcharo-Bunda, Mahakama ya Mwanzo Mugeta-Bunda, Mahakama ya Mwanzo Kenyana-Serengeti.
Nyingine ni Mahakama ya Wilaya Serengeti, Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Mugumu Mjini, Mahakama ya Wilaya Tarime, Mahakama ya Mwanzo Sirari-Tarime, Mahakama ya Wilaya Rorya, Mahakama za Mwanzo Ingri, Mahakama ya Mwanzo Riagoro na Mahakama ya Mwanzo Kinesi zote za Wilaya ya Rorya pamoja na Gereza moja la Wilaya ya Musoma.