ARUSHA-Kikosi cha Simba Queens kimeshindwa kutinga fainali ya michuano ya Samia Women’s Super Cup baada ya kupoteza kwa bao moja dhidi ya JKT Queens katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Queens ilitawala sehemu kubwa ya mchezo kipindi cha kwanza huku ikitengeneza nafasi kadhaa lakini ilishindwa kuzitumia.
JKT walipata bao hilo pekee dakika ya 29 kupitia kwa Jamila Rajabu ambaye alifunga kwa kichwa akimalizia mpira wa kona.
Kipindi cha pili Queens waliongeza kasi ya mashambulizi lakini JKT walikuwa makini kuhakikisha hawaruhusu nyavu zao kutikiswa.
Kocha Yussif Basigi alifanya mabadiliko ya kuwatoa Amina Bilal, Emeliana Mdimu na Dotto Evarist na kuwaingiza Asha Djafar, Fatuma Issa na Wincate Kaari.
Queens sasa itacheza na Fountain Gate Princess katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu utakaopigwa Machi 8 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.