DODOMA-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Husna Sekiboko imeridhishwa na ujenzi wa mradi wa Ofisi Mpya za Makao Makuu ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) unaotekelezwa katika Mtaa wa Vikonje Kata ya Mtumba Wilaya ya Dodoma mkoani Dodoma.
Kamati hiyo imetembelea na kukagua mradi huo Machi 12, 2025 ambapo ujenzi huo utafanyika kwa awamu nne na unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 53.7 hadi kukamilika.
Aidha, awamu ya kwanza ya mradi huo imefikia asilimia 45 na inatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2025.
Ujenzi wa awamu ya kwanza unahusisha jengo la utawala, studio za redio, televisheni, mitandao ya kijamii, pamoja na usimikaji wa mitambo yote muhimu ya uandaaji na urushaji wa matangazo, ikiwemo satellite uplink, transmission studio, na server-based system.
