Kamati ya Bunge yaridhishwa na uendelezaji vituo vya bunifu za TEHAMA nchini

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imesema,imeridhishwa na mradi wa uendelezaji wa vituo vya bunifu za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini.
Mwenyekiti wa kamati hiyo,Mhe.Moshi Selemani Kakoso ameyasema hayo leo Machi 16,2025 baada ya wajumbe wa kamati hiyo kufanya ziara katika Kituo Kikuu cha Ubunifu kilichopo makao makuu ya Tume ya TEHAMA, Upanga jijini Dar es Salaam.

"Tunaishukuru Serikali kwa uwekezaji wa vituo hivi vya ubunifu,kwa teknolojia ambayo itakuja kuwasaidia hasa wabunifu vijana.

"Pia, tunaipongeza Serikali kwa sababu tunavyo vituo ambavyo vimeanza kujengwa tofauti na huko nyuma ilivyokuwa."

Mheshimiwa Kakoso amesema kuwa, kwa sasa kuna zaidi ya vituo vinane nchini ambavyo anaamini vinakwenda kuwa msaada mkubwa kwa bunifu za vijana ambazo hazijaendelezwa.

"Serikali imeamua kufanya hivi, ili fursa hiyo iweze kuwa na mwendelezo."

Aidha, kamati imeielekeza Serikali kukamilisha vituo bunifu hivyo kwa wakati na kwa mujibu wa mikataba ambayo walisaini ili viweze kuhudumia vijana wenye bunifu mbalimbali nchini.

Jambo la pili, kamati imesema kujenga miundombinu ni kitu kingine, hivyo wanahitaji wataalamu ambao watakuja kuwafundisha vijana na kuendelea bunifu zao.

"Tunaweza tukawa na vituo vingi, lakini vikashindwa kupata ufanisi kwa sababu havina wataalamu."

Vilevile, kamati hiyo imeishauri Serikali kuwa na programu maalumu ambayo itakuwa ni muongozo wa kuendeleza programu za kuwasaidia vijana waweze kukuza ubunifu wao.

Jambo lingine ambalo wameliomba Serikali hususani kupitia Tume ya TEHAMA ni kwenda kutafuta makundi ya vijana ambao ni wabunifu.

"Tuna wabunifu wengi wapo mitaani, na bahati nzuri Serikali imeandaa kujenga chuo ambacho kitakuwa muunganisho wa bunifu za vijana."

Mwenyekiti huyo amesema kuwa, chuo hicho hakihitaji kuwa na degree, kwani mtu yeyote ataweza kupeleka bunifu zake ili ziweze kuendelezwa.

"Kwenye maeneo haya ni ya msingi sana, Serikali sasa itoke iende kuwatafuta vijana wale ambao wamefanya mambo mazuri."

Amesema, wana mifano hai ikiwemo watu waliobuni ubunifu wao wakaanzisha mradi wa umeme Mkoa wa Njombe.

"Lakini, pia tumeshuhudia vijana wamejenga helkopta Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Morogoro, lakini bunifu zao hazijaendelezwa kwa sababu kulikuwa hakuna mpango wowote wa Serikali kuendeleza."

Amesema, kupitia maeneo hayo, vituo hivyo vinapaswa kutoka kwa ajili ya kwenda kuwaibua hao vijana.

Mifumo ya Fedha

Wakati huo huo, Mheshimiwa Kakoso amesema,kwa sasa Taifa linahitaji bunifu za kisasa ambazo zitarahisisha ukusanyaji wa mapato na kufanya malipo kidijitali.

"Nchi yetu kwa sasa, tuna matumizi ya fedha za cash (taslimu), sasa tukipata vijana ambao wanatengeneza mfumo ambao utakuja kuendelezwa tutoke kwenye matumizi ya fedha taslimu.

"Itasaidia sana kwa nchi hii kukuwa,inawezekana kabisa kukawa na makundi ya vijana ambao wanaweza wakabuni mfumo ambao utasaidia hata makusanyo ya kodi yakapatikana kwa njia rahisi kwa sababu tutatoka kwenye matumizi ya cash.

"Haya ni mambo ambayo Serikali ikiyafanyia kazi itatufikisha mbali sana.Lakini, mwisho pamoja na jitihada ambazo zinafanywa na Serikali tunahitaji sasa hawa wabunifu waweze kulindwa, kuhifadhiwa bunifu zao, lakini kuziendeleza.

"Tunapoziendeleza, maana yake tunahitaji uwezeshwaji."

Serikali ikienda na mpango mkakati kama huo, Mwenyekiti huyo amesema,inaweza ikafanya vitu vikubwa zaidi.

"Hata, wenzetu wa China, walifanya hivyo na makundi ya vijana yamekuwa yakiendeleza bunifu zao za kawaida, lakini zimetoka kutoka za kawaida na kuwa zilizoenda kushika soko la nchi na baadaye kushika masoko ya Kimataifa."

Amesema, anaamini hayo yakifanyiwa kazi, bunifu za vijana wa Kitanzania zina uwezo wa kufika mbali.

Naibu Waziri

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema kuwa,ziara hiyo imelenga kujionea kituo hicho cha umahiri katika kukuza ubunifu wa kazi za TEHAMA kutoka kwa vijana wa Kitanzania.

"Ni mwendelezo wa kuhakikisha Tanzania ya Kidijitali inawezekana na ndiyo azima ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.  

"Sisi kama Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tunaendelea kusimamia maagizo yote ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa kuhakikisha vijana tunawatendea haki, katika kuona kwanza tunawakuza na mwisho wa siku kuja kuwahakikishia bunifu ambazo wamefundishwa kwa maana ya utaalam ambao watapatiwa basi wapate mahala pa kufanyia kazi."

Kwa siku ya leo,Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema, Kamati ya Bunge imetembelea kituo hicho ambacho kipo Dar es Salaam ikiwa ni moja kati ya vituo vingi ambavyo wanatarajia kuvijenga hapa nchini.

"Lakini, vituo nane katika mikoa nane vimeanza kufanyiwa kazi kwa maana ya ujenzi."

Amesema,lengo ni kuona vijana wengi wa Tanzania ambao ni wabunifu wanaacha kufanya kazi kiholela.

Naibu Waziri huyo anabainisha kuwa, Serikali inakwenda kurasimisha bunifu hizo ikiwemo wale waliobuni bunifu zao ili ziweze kutambulika rasmi.

Pia, amesema kuwa, hatua hiyo itasaidia kuvipatia usalama wa hali ya juu vifaa vyote vya TEHAMA.

"Kwa hiyo kituo hiki kitakuwa muhimu sana, vilevile tunatarajia hivyo vingine saba, mikoa ambayo tayari ujenzi unaendelea vyote vitakwenda kuwa vya manufaa makubwa katika nchi yetu."

Naibu Waziri huyo ameweka wazi kuwa, pia Serikali inatarajia kujenga shule kwa ajili ya ubunifu katika makao makuu ya nchi jijini Dodoma.

Dhamira ya Serikali kufanya hivyo, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema ni kuhakikisha Tanzania ya Kidijitali inafikiwa kwa haraka kwa ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

"Tunavyoendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya kiteknolojia, basi tuwe na wabunifu wetu wa ndani na tusiendelee kutegemea tu watu kutoka nje."

Katika hatua nyingine amesema, tayari kuna mwelekeo mzuri kwani kuna kiwand ambacho kimeanza uzalishaji wa bidhaa za TEHAMA.

Uzalishaji unaofanywa na kiwanda hicho kilichopo jijini Arusha ni kompyuta mpakato, simu na vifaa ningine vya kielektroniki.

"Kwa hiyo, Tume ya TEHAMA wanafanya nao kazi kwa karibu ili kuona bidhaa zinazotengenezwa zinakuwa katika ndani ya viwango vya Kimataifa."

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuweka mikakati thabiti ili vijana waweze kujifunza zaidi kwa ajili ya kuzifanya bunifu zao kuwa bora.

Ameongeza kuwa, vituo hivyo vinakwenda kuwapa vijana uwanda mpana ambao utawawezesha kubuni mifumo ya kusaidia ukusanyaji wa mapato na malipo mbalimbali kidijitali.

"Hii itatusaidia kwanza kupunguza uhalifu kwa sababu watu wataacha kutembea na maburungutu ya fedha."

Lakini, pia amesema, bunifu za vijana zitasaidia watu kuacha kukimbizana kwa kuhofia kufungwa kwa vituo vya kutolea huduma za kifedha.

"Kama mabenki ama mawakala, kila kitu kitakuwa kielektroniki."

Tume ya TEHAMA

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini, Dkt.Nkundwe Mwasaga amesema kuwa, kati ya vituo hivyo kuna vituo vya kukuza bunifu za vijana na vingine kwa ajili ya kutengeneza bidhaa.

Katika vituo vya kutengeneza bidhaa, Dkt.Mwasaga amesema, kimoja kipo TIRDO na kingine SIDO jijini Arusha.

Pia, amesema kwa upande wa makao makuu ya Tume ya TEHAMA jijini Dar es Salaam kuna vituo viwili.

Kati ya vituo hivyo, Dkt.Mwasaga amesema kimoja ni kwa ajili ya kukuza bunifu za vijana na kuna kituo kingine ambacho ni kati ya vituo 17 vya Umoja wa Mawasiliano Duniani.

Aidha, amesema kituo kingine kipo mkoani Lindi, Zanzibar, Tanga, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Arusha viwili na Dar es Salaam vitatu vyote vikiwa ni kwa ajili ya vijana.

"Kwa sababu, Tanzania sisi tumepata bahati ya kuwa na vijana wengi."

Dkt.Mwasaga anasema, idadi ya vijana kwa mujibu wa Sensa ambao ni kuanzia miaka 15 hadi 34 wapo milioni 21.

"Sasa hiyo idadi ni fursa kwetu, kwa hiyo hawa vijana wanatakiwa kupata uwezo wa kuweza kubuni uanzishaji wa kampuni na hizo kampuni ziweze kufanya mambo mawili makubwa.

"Kutengeneza kazi kwa vijana wenzao na kufanya Sekta ya TEHAMA itoe mchango mkubwa katika pato la Taifa la Tanzania."

Amesema, vituo hivyo vipo kwa ajili ya mbunifu yeyote bila kujali kiwango cha elimu yake.

"Tunachoangalia hapa ni ubunifu, huo ubunifu tunaukuza kwa miezi nane, kwa hiyo mbunifu atapata ofisi bure, atapata mafunzo bure,atakutanishwa na mabenki, atakutanishwa na wanasheria na atakutanishwa na kila hali ambayo itamfanya yeye kuwa kampuni."

Amesema, katika kipindi hicho atatumia rasilimali za kituo kama mtu akianzisha kampuni yoyote ambayo anaifungulia ofisi huko mtaani.

Dkt.Mwasaga ameeleza kuwa, Serikali imeanzisha vituo hivyo ili kuwaondolea vizuizi ambavyo wabunifu walikuwa wanakumbana navyo, hivyo kuwakatisha tamaa ya kusonga mbele.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news