NA LWAGA MWAMBANDE
MACHI 13,2025 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema,Serikali inaendelea na mkakati wa kufungua milango ya ujasiriamali kwa kutekeleza sera na programu mbalimbali zitakazowasaidia wananchi kuendana na soko la ajira ili kujiongezea kipato.
Ametoa kauli hiyo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya Amali ya Makomelo iliyopo Nzega mkoani Tabora ambayo ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 1.6 .
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa, Serikali iliamua kutenga kiasi cha shilingi bilioni 44.7 kwa ajili ya ujenzi shule za amali katika kila mkoa ili kuwawezesha Watanzania kupata elimu ya mafunzo maalum yatayowasaidia kujiajiri au kuajiri wengine na hatimaye kujikwamua kiuchumi.
Amebainisha kuwa,malengo ya Serikali ni kuwafikisha vijana kupata ujuzi ili ujuzi huo utumike katika kujipatia kipato na kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini, kwani sera ya elimu imesisitiza elimu ya ufundi mahiri kwa maana ya amali.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande licha ya kupongeza juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya elimu ufundi nchini,pia amewahimiza vijana kujitokeza kwa wingi katika vyuo vya ufundi (VETA) ili kupata ujuzi waweze kujiajiri. Endelea;
1. Watu wenye digirii, kasome ufundi VETA,
Kwa sababu digirii, huwezi pata mafuta,
Hili kama ukitii, huko mbele utapeta,
Hizi fani za ufundi, huwa ni ajira tosha.
2. Kwake Waziri Mkuu, hekima tunaipata,
Lake ndilo jungu kuu, mazuri tunayachota,
Elimu siyo ukuu, wakati tunatepeta,
Hizi fani za ufundi, huwa ni ajira tosha.
3. Hizi fani za ufundi, wengi pesa wanapata,
Na walipo hawagandi, kazi zinapitapita,
Ila pasipo ufundi, na digirii watota,
Hizi fani za ufundi, huwa ni ajira tosha.
4. Kweli shahada ni nzuri, hasa cheti ukipata,
Halafu yako safari, ukiwezesha kupata,
Utaona si vizuri, kuifikiria VETA,
Hizi fani za ufundi, huwa ni ajira tosha.
5. Shahada ukizijaza, nadharia ulopata,
Cha kufanya kutoweza, fursa zikipitapita,
Vema sana ukawaza, ya amali kuyapata,
Hizi fani za ufundi, huwa ni ajira tosha.
6. Ninaye ndugu rafiki, elimu ameipata,
Wale tunawaafiki, kwao tunapitapita,
Mbele kule hatufiki, bila mhuri kupata,
Hizi fani za ufundi, huwa ni ajira tosha.
7. Hao hasa ni wasomi, kotekote ukipita,
Wengine sio wasomi, ndivyo wanavyojiita,
Yeye maisha hakwami, kwa kukaa akijuta,
Hizi fani za ufundi, huwa ni ajira tosha.
8. Anao ufundi wake, kipato anakipata,
Hulivua joho lake, rangi akichotachota,
Na tena mkono wake, kwa kuta dari matata,
Hizi fani za ufundi, huwa ni ajira tosha.
9. Angekula yake tai, bila ya kazi kupata,
Hata pesa kunywa chai, asingeweza kupata,
Anakwenda hajidai, vile shahada kapata,
Hizi fani za ufundi, huwa ni ajira tosha.
10. Ya Mkuu Majaliwa, tusiyaache kupita,
Vyeti tulivyojaliwa, siyo elimu kufuta,
Wala hatujachelewa, kupata amali VETA,
Hizi fani za ufundi, huwa ni ajira tosha.
11. Kuna fani nyingi VETA, utakacho utapata,
Kubweteka watepeta, usotaka utapata,
Mfukoni utajuta, senti huwezi kupata,
Hizi fani za ufundi, huwa ni ajira tosha.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602