DAR- Kesi ya uhujumu uchumi ya msanii nicole yaahirishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni imeshindwa kuendelea na kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili msanii Joyce Mbaga, maarufu kama Nicole, kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Mbali na Nicole (32), mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Rehema Mahanhu.
Wawili hao walifikishwa mahakamani hapo Machi 10, 2025, na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhan Rugemalira, kwa mujibu wa Wakili wa Serikali, Rhoda Maingu.
Katika kesi hiyo iliyotajwa leo, upande wa Jamhuri umeieleza mahakama kuwa bado wanakamilisha upelelezi, hivyo wameomba ahirisho. Kutokana na maombi hayo, kesi imeahirishwa hadi Aprili 14, 2025.
Nicole na Mahanhu, ambao wako nje kwa dhamana, wanakabiliwa na mashtaka matatu, ikiwa ni pamoja na: Kuongoza genge la uhalifu Wanatuhumiwa kuendesha biashara haramu kwa lengo la kujipatia faida isiyo halali kutoka kwa jamii.
Kupokea amana bila leseni Inadaiwa kati ya Julai 2024 na Machi 2025, wakiwa eneo lisilofahamika ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, walipokea amana ya Sh 185,515,000 kutoka kwa jamii bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kuendesha mfumo wa malipo kinyume cha sheria – Washtakiwa wanadaiwa kuendesha mfumo wa malipo bila kuwa na leseni ya malipo inayotolewa na BoT.
Kesi hii inasubiri kuendelea kusikilizwa Aprili 14, 2025, huku upande wa Jamhuri ukiendelea na upelelezi.