Kidunda ni bwawa la kihistoria-Waziri Mkuu

MOROGORO-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Machi 05, 2025 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Bwawa la Kidunda litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita bilioni 190 ambalo linatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 335.8 hadi kukamilika kwake.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Kidunda, Wilayani Morogoro, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa bwawa hilo ambao umefikia asilimia 28.

Ujenzi huo ni utekelezaji wa maono ya Hayati baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alidhamiria kulijenga ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

“Bwawa hili lilikuwa katika historia tangu Serikali ya awamu ya kwanza na zilizofuatia, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuhakikisha maji ya kutosha yanapatikana, alielekeza kuanza kutekelezwa kwa mradi huu, na leo tumeweka jiwe la msingi, na anamatarajio makubwa na mradi huu.”
Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa ujenzi wa bwawa hilo ni utekelezaji wa dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha anamtua mama ndoo kichwani kwa kufikisha huduma ya maji safi na salama karibu na makazi ya wananchi.

Kadhalika Mheshimiwa Waziri Mkuu ameziagiza Mamlaka za Maji ziendelee kutoa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa na Serikali kwa gharama kubwa iweze kuwa endelevu.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa alisisitiza kuwa Wizara ya Maji ihakikishe inamsimamia mkandarasi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

“Tunataka mradi huu ukamilike kwa wakati, hatuna shaka na mkandarasi huyu, amefanya miradi mingi na kwa ufanisi”.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Maji kuhakikisha wananchi wanaozunguka mradi huo wanapewa kipaumbele pindi utakapokalika.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alielekeza kuwa maeneo yote yanayozunguka miradi ya maji wakazi wa maeneo hayo wapewe kipaumbele, Mheshimiwa Waziri simamia hili.”

Naye, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itasimamia mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati. “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ni suluhu ya matatizo yaliyoshindikana kama bwawa la Kidunda, ambalo linakwenda kutatua changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.”

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri alisema kuwa mradi huo unatarajiwa kuwa na mtambo wa uzalishaji umeme megawati 20, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 101 kutoka Kidunda hadi Chalinze kwenye gridi ya Taifa pamoja na ujenzi wa barabara kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilomita 75 kutoka Ngerengere hadi Kidunda.
Mradi huo utakapokamilika unatarajia kuboresha huduma ya majisafi kwa ajili ya matumizi ya majumbani, kilimo na viwanda kwa kuhakikisha upatikanaji wa muda wote katika mto Ruvu kwa kutiririsha wastani wa lita 24,000 kwa sekunde ,zitakazokidhi mahitaji ya maji hususani kwenye kipindi cha ukame.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news