NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewakutanisha viongozi wa ngazi ya juu wanaosimamia masuala ya kifedha mahususi katika Sekta ya Kibenki.
Lengo ni kujadili fursa zilizopo na namna ambavyo wanaweza wakatumia fursa hizo kutatua changamoto zinazoondoa tofauti zilizopo kati ya wanawake na wanaume katika upatikanaji wa huduma za kifedha nchini.
Kando ya mkutano huo unaoendelea makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam leo Machi 5,2025 Gavana Emmanuel Tutuba amesema,katika mkutano huo wanajadiliana juu ya namna ya kupunguza tofauti iliyopo kati ya masuala ya kijinsia yanayowezesha ujumuishi wa kifedha.
"Tunafahamu kwamba,Tanzania ni nchi ambayo imekuwa ikijipambanua kwa namna mbalimbali kufikia hatima ya kuwa na uwiano asilimia 50 kwa 50 katika shughuli mbalimbali.
"Hivyo katika masuala ya kifedha pia, tuna lengo la kufikia asilimia 50 kwa 50 kati ya huduma zinazofikiwa au zinazotumiwa na wanawake na wanaume ifikapo mwaka 2033."
Amesema, mwaka 2023 walifanya utafiti ambao unahusu walaji kuhusu namna huduma zinavyowafikia au zinavyotumika kwa wadau, kutokana na hizo huduma kulionekana kuna makundi matano ambayo hayajafikiwa na huduma vizuri.
"Lakini, kati ya yale makundi ukiyachambua utaona kuna mgawanyiko wa kundi la wanawake na wanaume kwa hiyo ukiyaunganisha sasa utakuta kwenye kundi la wanawake ilionekana bado hawajafikiwa sana na huduma za kifedha nchini."
Aidha, amesema kuna mikakati mbalimbali ambayo inafanyika ambapo Serikali na taasisi nyingine zinahakikisha huduma za kifedha zinajumuisha watu wote hasa kundi la wanawake ambalo limesahaulika.
"Kwa hiyo, mkutano wa leo unajadili fursa zilizopo na namna ambavyo tunaweza tukatumia fursa hizo kutatua changamoto zinazoondoa tofauti zilizopo kati ya wanawake na wanaume katika upatikanaji wa huduma za kifedha nchini."
Amesema, lengo hilo ambalo limewekwa katika kufikia huduma za kifedha mwaka 2033 limezingatia mazingira yaliyopo nchini, mikakati na Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Taifa (NBC),Bw. Theobald Sabi amesema, takwimu zinaonesha kwamba, wanawake bado wameachwa nyuma katika huduma jumuishi za kifedha.
Kutokana na changamoto hizo, Sabi amesema benki zinaendelea kuchukua hatua kadhaa ili kuwafikia wanawake wengi na biashara zinazowahusu wanawake.
Baadhi ya hatua ni pamoja na kuanzisha bidhaa ama huduma ambazo ni mahususi kabisa ambazo zinalenga kutatua matatizo yanayowakwaza wanawake ikiwemo dhamana, na changamoto ya lugha.
"Pia, kuna akaunti maalum ambazo zinaendana na mahitaji ya wanawake nchini.Kwa hiyo kuna nia ya dhati kuhakikisha ujumuishi wa wanawake unafanyika."