NA ARAPHA RUSHEKE
Mahakama Dodoma
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo hivi karibuni alikabidhi kompyuta mpakato (Laptop) na mashine za kuchapisha nyaraka kwa Mahakimu wapya saba wa Mahakama za Mwanzo zilizopo Mkoa wa Dodoma kwa ajiri ya kuwarahisishia utendaji kazi wa kila siku.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo na kushoto kwake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe Silivia Lushasi na kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Bw. Sumera Manoti wakiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wapya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma waliohudhuria hafla hiyo.
Makabidhiano hayo yalifanyika katika ukumbi wa Mahakama uliopo kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe Dkt. Masabo aliwakumbusha Mahakimu hao kuwa matumizi ya teknolojia kwa sasa yamepamba moto mahakamani, hivyo wanapaswa kuitumia vyema wanapotekeleza majukumu yao.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo akikabidhi vifaa aina ya Laptop na mashine ya kuchapia nyaraka kwa mmoja wa Mahakimu wapya Mkoa wa Dodoma.
“Mahakama mtandao imeshika kasi tofauti na zamani, nyie mmekuja kipindi ambacho kila kitu kipo kwenye teknolojia. Sote tunapaswa kuitumia teknolojia ipasavyo, hakikisheni mnatumia vizuri Primary Court App katika kusajili mashauri,” alisema.
Jaji Mfawidhi alieleza kuwa anaamini kuna wakati utafika watafanya kila kitu katika mtandao kama ambavyo Mahakama za Wilaya na nyingine zinavyofanya, hivyo Mahakimu hao wanatakiwa kujizoesha kuishi kwenye ulimwengu wa sasa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (katikati) na kushoto kwake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe Silivia Lushasi na kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Bw.Sumera Manoti wakiwa katika ukumbi wa Mahakama wakati wa hafla fupi ya kugawa vifaa kwa Mahakimu wapya.
Maofisa Utumishi Waandamizi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma wakifuatilia kwa makini hafla hiyo, wa kwanza kushoto ni Bw. Stanslaus Makendi na anefuatia ni Bw. Bakari Iddi.
Mhe. Dkt. Masabo alitumia fursa hiyo kuwahimiza Mahakimu hao kuzingatia ubora wa maamuzi yao na kuhakikisha wanafanya rejea ya sheria ili waweze kutoa hukumu bora.
Kwa upande wao kwa nyakati tofauti, Mahakimu hao walitoa shukrani kwa uongozi wa Mahakama kwa kuzingatia haja ya kuboresha mazingira ya kazi. Walisema kuwa vifaa hivyo vitawawezesha kufanya kazi zao kwa haraka zaidi na kuleta mapinduzi katika utoaji haki.