NA GODFREY NNKO
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeendelea kutekeleza mikakati kabambe katika kukomesha biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kudhibiti upatikanaji wa dawa za kulevya, kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya, kupunguza madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na kuimarisha ushirikiano na wadau kitaifa, kikanda na kimataifa.
Mikakati hii imelenga kuwezesha utekelezaji wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015, pamoja na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.
Tiba kwa Waraibu
Serikali kupitia DCEA kwa kutambua kuwa,
matumizi ya dawa za kulevya husababisha madhara mbambali ikiwemo madhara ya kiafya kwa watumiaji na jamii kwa ujumla imekuwa ikitoa huduma za tiba, utengamao, ushauri na unasihi kwa waraibu wa dawa za kulevya.
Maeneo ya msingi ya utekelezaji wa mkakati huo ni kuratibu matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya,kuandaa miongozo ya matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya na kufanya usimamizi shirikishi katika vituo vinavyotoa huduma za tiba, ushauri na unasihi kwa waraibu wa dawa za kulevya.
Kwa sasa hapa nchini kuna vituo 16 vya tiba saidizi kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT Clinics).
Vituo hivyo husimamiwa na Serikali na huwa vinahudumia waathirika wa dawa ya kulevya aina ya afyuni kama vile heroin na baadhi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya.
Waathirika wanaotibiwa kwenye vituo hivyo hutibiwa kwa kutumia dawa mfano Methadone.
Aidha,waathirika wanatakiwa kuhudhuria matibabu kila siku mpaka watakapomaliza matibabu ambapo huduma ya MAT hutolewa bure chini ya uangalizi wa wataalamu.
MAT Clinic Temeke
Miongoni mwa vituo hivyo ni Kliniki ya MAT Temeke iliyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Katika kliniki hii ambayo huwa inahudumia zaidi ya waraibu 900 kila siku, mmoja wa waraibu aliyejitambulisha kwa jina la Ally kutoka Temeke Mikoroshini anasema kuwa,uamuzi wa Serikali kuanzisha vituo hivyo umewasaidia.
"Asiyependa kushukuru huyo si mwema, mimi binafsi tangu nianze kupata dawa hapa nimeona mabadiliko makubwa sana kiafya, nilitumia dawa za kulevya kwa muda mrefu, lakini kwa sasa ninaonekana mwenye nuru katika jamii.
"Ninaishukuru Serikali kwa kutujali sisi waraibu, unaona wengi wetu tukimaliza kumeza dawa hapa, tuna nguvu ya kurejea katika jamii kwa sasa kujitafutia riziki."
Waraibu wanasemaje?
Kupitia vituo vya MAT, waraibu kama Ally huwa wanapata tiba ya Methadone ambayo inasaidia kupunguza utegemezi wa dawa za kulevya.
"Methadone inatusaidia sana kuondoa hamu ya kutumia dawa za kulevya."
Aidha, huwa inasaidia kupunguza madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Kudhibiti uhalifu
Mraibu huyo anathibitisha kuwa,matibabu hayo yamekuwa yakiwasaidia kupunguza tabia za kihalifu zinazohusiana uraibu ili kujipatia chochote kitu kwa ajili ya kununua dawa za kulevya.
"Kwa sababu uki-gratuate hapa unakuwa upo safi, hivyo usalama wa mali za watu katika jamii unakuwa haupo mashakani tena, tofauti na awali wakati uteja umekolea, teja unakwapua chochote kitu ili uweze kupata hela ya kununua dawa."
Ally anabainisha kuwa,kuna faida nyingi za vituo hivyo, huku akiwashauri wanaojificha kujitokeza kupata matibabu kwani MAT Clinics ni muhimu.
Pia, amesema zimekuwa zikisaidia waraibu kupata matibabu bora, kupunguza madhara ya uraibu na kuboresha ustawi wa jamii kwa ujumla.
Mraibu
Victoria Philipo Memba ambaye amezaliwa mwaka 1976 amesema, alijikuta ameingia katika utumiaji wa dawa za kulevya baada ya kushawishika na mwanaume ambaye aliingia naye katika mahusiano.
"Katika kupitapita kwangu nikazalishwa watoto wawili, nikabahatika kuishi na mzazi mwenzangu, bahati mbaya tukaja kuachana.
"Tulipokuja kuachana nikatembetembea nikabahatika kupata mwanaume, yule mwanaume ambaye nilikuwa ninaishi naye kumbe alikuwa ni teja.
"Mimi sikujua kama mwanaume ni mteja akawa akija anakuja na sigara ndani anavuta,ninamuona anasinzia siku nyingine akija anatengeneza vitu vyake, nikimuuliza hiyo nini anasema ni bangi.
"Tulienda...siku hiyo akanipa sigara bangi akaniambia nijaribu, nikajaribu tukawa tunavuta, tunalala.
"Siku nyingine kama sivuti ninamwambia mbona mimi sipati usingizi na mwili unaniuma? Ananiambia haya ni madawa kwa hiyo uendelee kutumia.
"Sasa tulipoendelea kutumia, siku moja kumbe yule mwanaume nilikuwa ninaishi naye alikuwa ni mwizi, nilikuwa sijui.
"Yule kaka akaja kukamatwa, katika kukamatwa nikafuatilia nikaambiwa mwanaume wako ni mwizi kamuibia mtu.
"Sasa nikawa sina hela ya kumtoa, sina nyuma wala mbele na uteja umeshakuwa mkubwa ikabidi sasa nianze kuingia mtaani nikikuta cha mtu ninachukua, nikikuta mtu kaanika nguo yake ninabeba ninauza ninapata hela ninavuta.
"Ikabidi niingie barabarani nikajiuza, nikipata hela ninavuta huku tena familia siijali, sijali watoto, sijali nani, nyumbani siendi nikawa maisha yangu ninalala magheto."
Victoria amesema, hali hiyo iliendelea hadi ikafikia hatua akawa anadhulumiwa kingono huku afya yake ikiendelea kuzorota.
Pia amebainisha kuwa, kuzorota huko watu walianza kumkejeli kila anapopita huku akiitwa majina ya hovyo mara hilo teja linapita.
"Nyumbani nikirudi familia inanishangaa, mbona uko hivyo, unaumwa? Siumwi, wakikaa vibaya ninaiba ikawa maisha yakawa magumu sana, tumekwenda mwaka 2015 hivi wakaniambia Temeke kuna Methadone imefunguliwa.
"Nikasema sawa nitaenda kupata dawa maana hali imekuwa mbaya sana, hata kama ukienda mtaani unalia shida unaonekana teja tu."
Victoria amesema, baada ya kufika MAT Clinic Temeke alianza kupata huduma ambazo zilimpa mwanga katika maisha yake.
"Huduma hizi zimetusaidia sana, kwa sasa ni tofauti kabisa na tulipokuja mwanzo hapa, tuko tofauti.
"Kwanza sasa hivi tunajielewa, familia inatujali, sasa hivi kila tubapokwenda watu wanatukumbuka sasa hivi, hata mtu akikuona unatembea mtaani anapenda akuone aongee na wewe."
Amesema, kutokana na thamani hiyo ambayo wameanza kupewa na jamii wanaishukuru Serikali kwa huduma hiyo ya Methadone.
Pia, amesema kupitia huduma hiyo wamekuwa wakipewa elimu kuhusu namna ya kutumia vipaji vyao ili kushiriki katika shughuli za uzalishaji katika hamii kujiletea maendeleo.
"Tunawaomba wale ambao hawajawahi kutumia dawa za kulevya wasitumie dawa za kulevya, dawa za kulevya siyo nzuri na kama kuna watu ambao wako mitaani dada, kama bado wanajifichaficha tunawaomba waje kunywa Methadone.
"Methadone inawezekana, Methadone inaponyesha na ni tiba mbadala miaka miwili mpaka mitatu."
Asante DCEA
Mraibu huyo ameishukuru DCEA kwa kuonesha upendo kwao kwani sasa wameona nuru mpya maishani mwao.
Awali, amesema alikuwa hana mwelekeo wa maisha kutokana dawa za kulevya kuharibu ndoto zake na afya.
Mathalani, kwa sasa amesema ana uhakika wa kipato na pia malazi yake yana ubora tofauti na miaka kadhaa iliyopita.
"Kwa hiyo ninashukuru kwa sasa kwa sehemu ninajiweza, hata ukienda kuomba kitu au kukopa watu wanakuwa na imani nawe tofauti na huko nyuma."
Kamishna Matikila
Machi 7,2025 wanawake kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) waliwatembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wanawake waraibu wa dawa za kulevya katika Kituo cha MAT Temeke.
Ziara hiyo iliongozwa na Veronica Octavian Matikila ambaye ni Kamishna wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
"Leo tumeona ni vema tukasherehekea vilele hivi vya Sherehe ya Siku ya Wanawake Duniani pamoja na wanawake ambao ni waraibu wanaopata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke.
"Kwa nini tumeamua kuchagua hospitali hii? Ukiangalia katika mamlaka tuna misingi minne ambayo tunaifanyia kazi.
Kamishna Matikila amesema,msingi mmoja wapo ni kuhakikisha wanasaidia kupunguza madhara ya dawa za kulevya.
"Tunapunguza madhara ya dawa za kulevya kwa kutoa tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya kwa kupata huduma katika hospitali kama MAT ambayo hiyo inapatikana katika Hospitali ya Temeke ikiwa ni kituo kimoja wapo kinachotoa huduma za Methadone.Lakini,kwa pamoja tunafanya kwa kupitia nyumba za upataji nafuu.
"Tumepata nafasi ya kukaa na kuongea nao,na wametuelezea ni historia gani ambayo iliwapelekea wao wakaanza kujiingiza katika uraibu wa dawa za kulevya.
"Lakini, pia kuwarejeshea tumaini na imani kwamba Serikali inawathamini, inawapenda japo kuwa kama mamlaka tunapambana na tuko kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
"Hatuna nia ya kutokuwajali raia wetu, raia wa Tanzania wana thamani kwa hiyo kama wanawake tumekuja kuwatia moyo."
Serikali inawathamini
Pia, Kamishna Matikila amewataka waraibu hao kutambua kwamba,Serikali inawathamini na imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kuweza kuwasaidia waweze kurudi katika hali zao za kawaida ili waweze kuwa pia na tija katika uzalishaji kiuchumi, lakini pia na thamani kijamii.
"Tunawaasa wanawake wote ambao kwa namna moja ama nyingine wameingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya msiogope, njooni Serikali imewekeza pesa za kutosha, imeweka utaratibu wa kutosha kuweza kuwasaidia, kuweza kurudi na kuweza kuwa katika hali yenu ya kawaida.
"Tiba dhidi ya dawa za kulevya ipo, msione aibu njooni japokuwa kuna ile hali ya kujiona kuna unyanyapaa.Lakini, sasa hivi jamii inaelewa njooni msiogope tuko pamoja kusaidiana, vita hii si ya mtu mmoja.
"Tuko pamoja tunashirikiana kusaidiana, Serikali inatoa pesa na kwa namna hiyo tunamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kwa namna moja ama nyingine toka ameingia madarakani amewekeza kiasi kikubwa cha pesa."
Pia, Kamishna Matikila amesema, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwatia moyo dhidi ya mapambano ya dawa za kulevya.
Kwa hiyo, amesema jambo ambalo wanalifanya ni kuendelea kuunga mkono jitihada za Awamu ya Sita za kuhakikisha Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana.
"Ukiangalia kauli mbiu ya mwaka huu ni kumwezesha mwanamke na msichana kufikia haki yake, kufikia masuala ya usawa na pia kuwatia moyo.
"Hilo tumelifanya kwa kupitia huduma ambayo tunaitoa,kuna suluhisho twende huko huko kwenye suluhisho."
Endeleeni kupambana
Aidha, amewapongeza malikia hao wa nguvu huku akiwataka kuendelea kupambana,kwani mamlaka licha ya kutoa tiba, pia inaendesha programu za kuwajengea uwezo waweze kujitegemea wakirudi katika jamii.
"Kwa hiyo, msijisikie vibaya, msijione wapweke,msijione mmeachwa wanawake tunaweza kwa kushikamana, tunaweza kwa kuamua sisi wenyewe na tunaweza tukajibadilisha sisi na tukabadilisha jamii yetu."
Amesema, lengo ni kuwa na jamii iliyo salama kwani jamii salama haina maana kwamba haijawahi kukutana na changamoto.
"Lakini, jamii iliyo salama ni ile jamii ambayo hata baada ya kukutana na changamoto huwa inakuwa na njia rahisi na njia salama za kushinda hizo changamoto na kuishi maisha ambayo ni salama baada ya hapo."
Pia, Kamishna Matikila amesema,Serikali imeweka Sera ambayo inatoa muongozo kuwa malezi dhidi ya dawa za kulevya yanaanzia ngazi ya kaya.

Katika ziara hiyo, wanawake kutoka DCEA waliwapatia zawadi mbalimbali wanawake wenzao ambazo zinabeba utu wa mwanamke kuonesha kuwa wapo pamoja na wanajaliana.
Vilevile ametoa wito kwa wanawake ambao wapo nyumbani huku wakiwa waraibu wa dawa za kulevya kujitokeza ili kupata huduma za methadone ili kurejesha matumaini yao upya.
Msikate tamaa
Kamishna huyo amesema kuwa, kwenye maisha wanasema kuna kuanguka,kuna kunyanyuka na kuna kupanda.
"Changamoto hii ni kubwa, wala si ndogo. Lakini, pia ni aina ya changamoto ambayo ikikupata unajiuliza mara mbili, niende nisiende.
"Lakini, hatujui tulianzaje, lakini ukianza kulitumia haijifichi, unaweza ukawa unabadilisha maeneo, lakini madhara ya matumizi ya dawa za kulevya ni tofauti na madhara ya mambo mengine.
"Lakini, pia madhara ya dawa za kulevya hauwezi kuyamaliza ukiwa peke yako ukiwa umejifungia."
Amesema, licha ya jitihada za kupambana na dawa hizo ikiwemo kutoa elimu pia suala la kushughulikia madhara wamejikita huko.
Amesema, Serikali imeendelea kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika kupambana na dawa za kulevya ikizingatiwa kuwa thamani ya rai mmoja ni kubwa.
Amesema, kutokana na uthamani huo ndiyo maana Serikali imehakikisha afya za raia wake zinalindwa kwa gharama yoyote.
Kamishna huyo amesema, pengine Serikali inawekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa kuwa,raia mmoja ana thamani kubwa.
"Raia mmoja ni wa thamani kubwa sana kwa nchi, hivi mnafahamu kuwa kwa nchi inaweza kwenda vitani kwa raia wake mmoja? Sasa vita si lazima kuchukua silaha, hapana kwani hata kutoa pesa kununua dawa, kuanzisha kituo watu wakaja wakapata matibabu ni vita ya kiafya.
"Serikali inawajali sana na ukiangalia kwa kiasi kikubwa, Rais wetu wa Awamu ya Sita amewekeza kwa kiasi kikubwa sana kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
"Licha ya wakati mwingine vipaumbele vya Serikali vinatofautiana kama sasa hivi tupo kwenye uchaguzi, lakini kwenye suala la matibabu dhidi ya madhara ya dawa za kulevya, Serikali haijaacha kutoa huduma."
Kutokana na hatua hiyo, waraibu hao walimpongeza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa moyo wa upendo kwao.
Aidha,Kamishna Matikila amesema kuwa, ujasiri wa wanawake hao kujitokeza hadharani kwa ajili ya kupata matibabu unadhirisha wao ni wanawake wa nguvu.
"Kwa sababu akiathirika mwanaume anaweza akawa ni mwanaume peke yake ameathirika, lakini akiathirika mwanamke mmoja, madhara yanakwenda kwa zaidi ya mtu mmoja.
"Kwako wewe mwenyewe,kwa mtoto utakayemzaa, kwa mume, kwa mzazi na kwa jamii. Hivi,unajua unaweza kumuacha mama na watoto saba na akalea?.
"Acha Baba na mtoto mmoja, patakucha kweli asubuhi? Maana yake bila mama mambo hayaendi, kwa hiyo msije mkafikiria kukata tamaa, huwa tunapata matatizo, lakini hakuna kukata tamaa mbele kuna suluhisho."
Daktari Mtui
Kwa upande wake Frida Thobias Mtui ambaye ni daktari wa magonjwa na afya ya akili katika Kituo cha Methadone Temeke amesema kuwa, kituo hicho kimeanzishwa miaka 11 iliyopita.
Ndani ya miaka hiyo, Dkt.Mtui amesema wameendelea kutoa huduma ambapo zaidi ya waraibu 3,500 wamehudumiwa.
"Kwa sasa hivi wagonjwa ambao wanapata huduma ni kama ni zaidi ya 900 ambao katika hao asilimia 3 ni wanawake."
Ukiachana na huduma za Methadone amesema, pia huwa wanatoa huduma za upimaji wa magonjwa ya VVU na homa ya ini.
Amesema, wale ambao wanagundulika wana VVU wamekuwa wakipewa huduma za ARVs, matibabu ya kifua kikuu na wenye homa ya ini huwa wanapelekwa vituo husika.
Pia, wamekuwa wakiwapa ushauri nasihi kuhusu kuacha matumizi ya dawa za kulevya na vilevi vingine.
"Na tumekuwa tukiwapa huduma ya kuwakutanisha na familia kwa kuita vikao kwa ajili ya kuja kuendelea kuwaunga mkono na kuwarudisha ili waweze kuungwa mkono na jamii."
Daktari Kileju
Kwa upande wake,Dkt.Joyce Kileju ambaye ni daktari anayehusika na huduma za tiba na utengamao kwa waraibu, amesema uanzishwaji wa kliniki hiyo ni utekelezaji wa nguzo ya tatu ya mamlaka katika kupunguza madhara yatokanayo na utumiaji wa dawa za kulevya.
Vilevile amesema,MAT Clinic Temeke ni kituo kikubwa ambacho kinasaidia sana katika kazi za mamlaka.
"Unaweza kujiuliza mimi ninapambanaje, kwani mimi ninapambana? Lakini mnapambana katika kukubali kuja kukitumia hiki hiki kituo, kupunguza madhara tayari mmeisaidia mamlaka katika kufanya kazi nguzo yake ya tatu."
Amesema kuwa,kituo hicho ambacho kilianzishwa miaka 11 iliyopita kilikuwa ni kituo cha tatu baada ya Muhimbili na Mwananyamala.
"Tunajua Temeke yetu hii imechafuka sana na hayo matumizi ya dawa za kulevya, lakini kama mamlaka tungeleta hiki kituo halafu na ninyi mkawa hamna mwitikio ina maana tungekuwa tumefanya kazi bure.
"Kwa hiyo, kuleta kituo hapa na ninyi mmekubali, mmeunga mkono mnaendelea kusambaza hizi habari kwenye jamii, hata wengine ambao hawajakubali msikate tamaa, muendelee kuwachukua wanawake wenzenu kwa ajili ya kuwakomboa, kukomboa roho za wananchi.
"Kwa hiyo, mnapokomboa roho za wananchi na nyie mnakomboleka."
Kwa sasa, kituo hicho kinahudumia wanawake 40 idadi ambayo ni sawa na asilimia 3 ya waraibu wanaohudumiwa.
Aidha, idadi hiyo ya wanawake inatajwa kuwa ni kubwa kujitokeza kupata huduma kituoni hapo ikizingatiwa vituo vingine wakati mwingine huwa havina mwanamke hata mmoja.
Hali hiyo, inachangiwa na wengi wao kutojitokeza au kujificha kwa hofu ya kupata aibu jambo ambalo wameshauriwa waachane nalo.
"Kwa hiyo, wale ambao wamehitimu na kutafuta wenzao katika jamii na kuwaleta ninawapongeza sana."
Mbali na mamlaka kuwapongeza wahudumu wa kituo hicho, pia imeahidi ushirikiano zaidi katika kuendelea kuleta dawa na miongozo.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Makala
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)