ZAZIBAR-Ofisi ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Zanzibar kwa kushirikiana na Ubalozi wa Heshima wa Brazil uliopo Zanzibar, walikutana na wadau na viongozi wa Taasisi za umma na binafsi kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano na Brazil kupitia diplomasia ya michezo na maandalizi ya mechi ya kirafiki kati ya Maveterani wa soka wa Zanzibar na Brazil.
Mchezo huo wa kihistoria wa kirafiki kati ya Mashujaa wa Zanzibar na Brazil, unatarajiwa kufanyika mwezi Juni 2025 mjini Zanzibar. Mchezo huo wa Kirafiki utawaleta nchini nyota kadhaa wa zamani wa soka wa Brazil kama vile Ronaldinho Gaúcho na Romário de Souza.
Kuja kwa nyota hao wa mpira wa miguu kunatarajiwa kuitangaza Zanzibar Kimataifa kama kituo muhimu cha michezo duniani pamoja na kuchochea ukuaji wa shughuli za utalii, biashara, kuibua vipaji vya mpira kwa vijana wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na kujenga daraja la ushirikiano kwa vilabu vya michezo kati ya Brazil na Zanzibar.
Kikao hicho kilichofanyika tarehe 18 Machi , 2025 kilihudhuriwa na wadau kutoka Wizara ya Afya, Habari, Utamaduni na Michezo, Wizara ya Utalii, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Mashirika ya Michezo, Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Idara ya Zima-Moto. Taasisi ya Utalii Zanzibar (ZATO) Shirikisho la mpira Zanzibar-ZFF.