DAR-Zaidi ya Mawakili 300 wa Serikali wanatarajia kukutana jijini Arusha kwa ajili ya mafunzo ya siku tano yanayolenga kuwanoa katika masuala mbalimbali ikiwemo mikataba ya kimataifa na ya ndani ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 19, 2025 jijini Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari wakati akielezea juu ya mafunzo hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Machi 24 hadi 28, 2025.
Johari amesema mafunzo hayo yanalenga pia kuboresha na kuimarisha uwezo wa mawakili wa serikali nchini katika maeneo ya usuluhishi wa migogoro hasa ya kibiashara na kwamba yataendeshwa na wanasheria wabobezi kutoka ndani na nje ya nchi.
“Eneo ambalo mawakili hawa watafundishwa ni katika masuala ya haya mikataba ambayo siyo ya kimataifa hata ya ndani ya nchi, watajua nini hasa misingi ya mikataba hiyo, unatakiwa kuwa na ujuzi gani maalum katika kuendesha mijadala kwenye meza ya majadiliano, miiko na vitu vya kuzingatia katika meza hiyo.
“Kwa hiyo umahiri huo tukiuboresha na sisi kama wanasheria tukijikumbusha na kujifundisha tukawa wabobezi itasaidia uwezo wetu katika meza ya majadiliano ya mikataba hii kuimarika, na kama tunavyofahamu Rais wetu anazidi kufungua nchi na kuna ongezeko la wawekezaji maana yake mikataba itaendelea kuwa mingi hivyo sisi wanasheria lazima kuhakikisha tunakwenda na kasi hiyo,” amesema na kuongeza;
“Kila mtu anafahamu kuwa dira ya mwaka 2050 ilizinduliwa pamoja na mambo mengi yanaliyozungumzwa kwenye dira hiyo, ni lazima ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuboresha huduma zake katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya mikataba ndio maana tunasema mafunzo hay ani muhimu,” amesema.
Amesema, pia mafunzo hayo yatazungumzia usuruhishi wa migogoro hasa ya kibiashara kwani wanajua katika mikataba mingi inaingia kwenye migogoro, hivyo mawakili wakipata ujuzi ni wazi kuwa watakuwa mahili katika kushughulikia kesi za migogoro hiyo.
Johari amesema, pia mafunzo hayo yatajikita pia katika suala nzima la utungaji wa sheria na uandishi wa sheria ambao ni taaluma yenye namna yake, misingi, kanuni na utaalamu wa kuandika.
“Tunataka pia kuangalia jukumu la wakali au mwanasheria katika kuuvaa uzalendo, kulinda maslahi pamoja na usalama wa Taifa ni nini, kwa sababu wasipofahamu hilo wanaweza wakajikuta wanaingia kwenye matendo ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wa Taifa au kuleta athari katika maslahi ya taifa yetu kiuchumi au kijamii.”