Mchungaji Mashimo ahukumiwa kwenda jela

DAR-Mahakama ya Wilaya Kinondoni jijini Dar es Salaam imemhukumu Mchungaji Daud Nkuba maarufu kwa jina la Komando Mashimo (Mchungaji Mashimo) kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili kati ya matatu aliyokuwa akishtakiwa nayo.
Mashino ametiwa hatiani kwenye mashtaka ya kuingia kwa jinai na kuharibu mali na imemuachia huru kwenye shtaka la kutishia kwa vurugu.

Mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka matatu ambapo upande wa Jamhuri umethibitisha makosa mawili na kushindwa kuthibitisha shtaka la kutishia kwa vurugu kama walivyomshitaki.

Hukumu hiyo imesomwa leo Machi 18, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhan Rugemalila baada ya upande wa Jamhuri kuthibitisha makosa dhidi ya mshitakiwa pasi na kuacha shaka yoyote.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Rugemalila amesema, ameridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa Jamuhuri na vielelezo ambapo wameweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo mawili.

Lakini, Hakimu amemuachia katika shtaka la tatu kwa kuwa Jamuhuri wameshindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.

“Mshtakiwa katika kosa la kuingia kwa jinai Mahakama inakupa adhabu ya kwenda jela miezi sita, kosa la kuharibu mali mahakama inakutia hatiani na kukupa adhabu ya kwenda jela miaka miwili.

"Pia,mahakama inakuachia huru kwa kosa la kutishia kwa vurugu kwa sababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi yako, hivyo utatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani,"amesema Hakimu Rugemalila.

Mshtakiwa kabla ya kusomewa adhabu yake hiyo alipewa nafasi ya kujitetea ambapo aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Rhoda Kamungu uliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa kama sheria inavyoelekeza ikawae fundisho kwake na jamii nzima.

Awali ilidaiwa Novemba 22, 2023 huko katika maeneo ya Mbezi Luis Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam,Mchungaji Mashimo aliingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na Frola Mwashaa.

Pia,Mshitakiwa katika kipindi hicho kwa makusudi na kinyume cha sheria aliharibu ujenzi wa nyumba iliyoko maeneo ya Mbezi Luis ambayo ni mali ya Frola Mwashaa. Katika shtaka la tatu,inadaiwa alimtishia Ramson Vicent kwa vurugu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news