NA LWAGA MWAMBANDE
IJUMAA ya Machi 19, 2021 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliandika historia ya namna yake kwa kuwa na Rais wa kwanza mwanamke ambaye ni Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Dkt.Samia aliapishwa siku hiyo,baada ya kifo cha Rais Dkt.Jonh Pombe Joseph Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Leo Machi 19,2025 imetimia miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt.Samia akiwa madarakani.
Dkt.Samia ni mama na kiongozi anayechukuliwa kuwa mwenye mtazamo chanya wa mabadiliko katika nyanja mbalimbali kuanzia kisiasa,kiuchumi na kijamii.
Katika kipindi cha miaka minne kuna mambo mengi ambayo ameyafanya kwa ustadi mkubwa ikiwemo alivyoweka historia ya kusimamia mapambano dhidi ya UVIKO 19 kwa kuhamasisha hatua mbalimbali za kiafya na chanjo.
Aidha, Rais Dkt.Samia amekuwa kinara katika kutekeleza miradi mikubwa ya barabara, nishati, reli, elimu, afya, maji na mingineyo kote nchini.
Pia, Rais Dkt.Samia amekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha uchumi licha ya changamoto ambayo iliikumba Dunia kutokana na vita kati ya Urusi na Ukraine, alionesha utulivu na umahiri mkubwa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Juhudi hizo zilienda sambamba na uwazi katika utekelezaji wa miradi serikalini huku akiongeza ushirikiano wa kiuchumi na mataifa mbalimbali duniani.
Vilevile, Rais Dkt.Samia amekuwa mstari wa mbele katika kukuza demokrasia na haki za binadamu ikiwemo kuruhusu uhuru wa vyombo vya habari.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande kwa juhudi hizo ameendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia huku akibainisha kuwa, miaka minne alianza na ameweza. Endelea;
1. Alianza ameweza, hata amepitiliza,
Sisi tunampongeza, jinsi nchi amekuza,
Nyanja zote kasogeza, ubora ameongeza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza,
2. Ni kubwa historia, mambo ametekeleza,
Hayo nasi yabakia, huku tukimpongeza,
Ni ghafla alianzia, Tanzania kuongeza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
3. Wakasema mwanamke, kweli huyu ataweza,
Acha mpini ashike, na vema kutuongoza,
Vizuri awajibike, makubwa ameyaweza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
4. Alianza na UVIKO, wakati inachakaza,
Wasiwasi ukaweko, Rais ataiweza,
Akauleta mwamko, kuchanja tukakuweza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
5. Miradi kimkakati, ndio ilikwishaanza,
Yote ikawekwa kati, huku ikimuuliza,
Hii imempa chati, safi sana kueleza,
Miaka mine Samia, kazi ameshamaliza.
6. SGR twajua, inaenda yapendeza,
Utamu tushaujua, Dar-Dom twateleza,
Macho imetufungua, kwamba Rais kaweza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
7. Ujenzi waendelea, Isaka kutoka Mwanza,
Lengo kuisogelea, Rwanda ndiko twawaza,
Ni Rais achochea, kazi kiendeleza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
8. Lile la Nyerere Bwawa, umeme kuutandaza,
Mambo yamekwenda sawa, tunamalizamaliza,
Umeme ni wa kugawa, kote tukiusambaza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
9. Hapohapo, angalia, REA ikitutuliza,
Yote Rais Samia, mambo anayaongoza,
Kwamba kote Tanzania, umeme kuusambaza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
10. Miradi ya usafiri, mingi aitekeleza,
Barababara zawa nzuri, madaraja atandaza,
Hii kazi siyo siri, sana anaendeleza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
11. Mfano Darisalamu, kotekote yapendeza,
Miradi yote mitamu, jiji lizidi pendeza,
Mwendokasi ni karamu, jinsi utajisambaza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
12. Dodoma nako kutamu, kunazidi kupendeza,
Hizi ni zake salamu, wote waliuombeza,
Eapoti inatimu, barabara aeneza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
13. Sasa twende kwa elimu, nani anayemkwaza,
Hili sote twafahamu, shule alivyosambaza,
Madarasa ya elimu, walimu ameongeza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
14. Kidato cha Sita shule, za wasichana kaweza,
Sasa anakwenda mbele, wavulana kuwasuza,
Madarasa mengi shule, nchini amesambaza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
15. 4R kazishusha, hizo azitekeleza,
Maridhiano yakosha, watu wanajieleza,
Ustahimilivu tosha, hebu nchini chunguza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
16. Afya bado sijasema, ubora ameongeza,
Ule uzazi salama, sana anasisitiza,
Vifaa tiba salama, kote anavieneza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
17. Hivi ni sekta gani, ambayo imepoozaa,
Zote zenda kileleni, jinsi anatuongoza,
Utalii wa mbugani, Royal Tour katangaza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
18. Yake Rais Samia, mengi yanajieleza,
Kuongoza Tanzania, na mengi kutekeleza,
Kazi zilizosalia, hakika tatekeleza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
19. Rais kweli hamasa, wanawake wanaweza,
Vema kupatiwa fursa, mema kuyatekeleza,
Huu ndio ukisasa, na nchi kuendeleza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
20. Heri tunamtakia, kazi aweze maliza,
Atumike Tanzania, mbele akitusogeza,
Uchumi weze fikia, viwango vya kuongoza,
Miaka mine Samia, alianza ameweza.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602