Mradi wa Huduma za Tahadhari za Hali Mbaya ya Hewa wazinduliwa rasmi

DODOMA-Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe. David KIhenzile (Mb) akimwakilisha Waziri wa Uchukuzi amezindua rasmi Mradi wa Huduma za Tahadhari za Hali mbaya ya Hewa (Early Warning for All- EW4ALL), Jijini Dodoma, tarehe 19 Machi 2025.

Mradi huo unafadhiliwa na nchi ya Denmark ukiwa na lengo la kuhakikisha kuwa kila mtu anafikiwa na huduma za tahadhari hivyo kulindwa dhidi ya matukio ya hali mbaya ya hewa ifikapo mwishoni mwaka 2027.
Katika hotuba yake, Mhe. Kihenzile alisema, “Uboreshwaji wa huduma za tahadhari dhidi ya hali mbaya ya hewa ni muhimu sana hasa kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, kwani uchumi wa nchi hizi unajengwa zaidi na sekta za kijamii na kiuchumi zinazotegemea sana hali ya hewa, na kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ambayo yamesababisha matukio ya hali mbaya ya hewa kuwa ya mara kwa mara na ya hatari zaidi, hivyo kuwepo kwa mradi huu ni tija kwa Taifa letu.”

Aidha, Mhe. Kihenzile aliongeza kuwa katika kufikia malengo ya mradi nchini, ushirikiano kati ya washirika wote wanaotekeleza mradi huu unahitajika. 

“Nitoe rai muendelee kuwa na mtazamo wa pamoja na kuhakikisha kuwa shughuli zinazotekelezwa zinafanyika kwa ufanisi ili kufikia matokeo na malengo yaliyokusudiwa. 

"Ni muhimu kuboresha usambazaji wa taarifa za tahadhari kwa njia zenye tija hasa kwa gharama nafuu ili kuhakikisha kuwa watu wote, wakiwemo wanaoishi maeneo ya vijijini, wanafikiwa na taarifa hizi.”
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Kanali. Selestine Masalamado alisema Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu ina jukumu kubwa la kuratibu masuala mbalimbali katika ngazi ya kitaifa ambapo moja ya majukumu yake ni kuratibu hatua za kukabiliana na majanga mbalimbali yakiwemo majanga yatokanayo na matukio ya hali mbaya ya hewa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Hali ya Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dk.Ladislaus Chang'a alisema Ripoti ya Tathmini ya Sita ya Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) imeainisha bayana kuwa matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo Mvua kubwa, Joto kali, Upepo mkali, Mafuriko, Ukame na Vimbunga yameongezeka na yanatarajiwa kuendelea kuongezeka kwa idadi na ukubwa kadri ambavyo joto linaongezeka, na kusababisha majanga makubwa.

Aidha, Dkt. Chang’a aliongezea kuwa “Leo hii tutatoa ripoti yetu ya tathmini ya hali ya Klaimatolojia kwa mwaka 2024 iliyoandaliwa na TMA na pia wasilisho maalaumu litafanywa katika warsha maalumu itakayofanyika leo na kesho sanjali na uzinduzi huu”.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alisema WMO itaendelea kushirikiana na TMA pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha lengo linafikiwa na kuhakikisha watanzania wote wanafikiwa na huduma za tahadhari za hali mbaya ya hewa.
Balozi wa Denmark alielza kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi tano za Afrika ambazo zimechaguliwa kutekelza mradi huu kwa ufadhili wa Denmark, na hii ni kutokana na ushirikiano wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na Denmark katika masuala ya huduma za hali ya hewa.

Mradi huu unatekelezwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Washirika wengine katika ngazi ya Kitaifa na ya Kimataifa ambao ni Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Usimamizi wa Maafa, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Majanga (UNDRR), Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Shirika la Mawasiliano la Kimataifa (ITU), Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS), na Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (IFRC).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news