Muziki wa Singeli kutambulishwa Kimataifa

DAR-Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema Serikali imedhamiria na imeanza safari ya kuupeleka muziki wa Singeli kimataifa ili uorodhesheshwe katika utamaduni usioshikika kwenye Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).
Msigwa amesema hayo wakati akifungua rasmi warsha ya Uteuzi wa Urithi wa Utamaduni Usioshikika iliyoendeshwa na UNESCO katika ukumbi wa Hoteli ya Four Points uliopo Posta jijini Dar es Salaam ikikusanya wadau mbalimbali wa muziki, viongozi wa Serikali na wataalamu wa utamaduni.

Msigwa amefungua warsha hiyo Machi 24, 2025 ambapo amesema muziki wa Singeli una uwezo mkubwa wa kuchochea maendeleo na kuleta umoja katika jamii ikiwa utazingatia maadili na kuakisi utambulisho wa Taifa.

"Wataalamu wetu wakina Dokta Kedmon Mapana na Wataalamu wa Vyuo Vikuu wamefanya utafiti wakabaini pasipo mashaka kwamba nyumbani kwa muziki wa Singeli Duniani kote ni Tanzania"Amesema Msigwa.

Aidha, Msigwa aliitaka BASATA, chini ya Katibu Mtendaji Dkt. Kedmon Mapana kuhakikisha inasimamia kikamilifu maadili katika muziki wa Singeli ili kuufanya uwe na hadhi inayostahili mbele ya dunia.

Msigwa pia alitoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha wanalinda, kutunza na kuenzi maadili pamoja na mila na desturi za Kitanzania ambazo ni hazina muhimu kwa taifa.

Warsha hii ya Uteuzi wa Urithi wa Utamaduni Usioshikika inalenga kuweka msingi thabiti wa kutambulika kwa muziki wa Singeli kimataifa, huku ikiendelea kufanywa kuwa daraja la kuunganisha watu na kukuza utamaduni wa Tanzania.

Naye Seleman Jabiri maarufu kwa jina la Msagasumu ameishukuru Serikari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuupa kipaumbele mziki wa Singeli na kuwa kama Alama ya Utambulisho wa Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news