Mwenyekiti wa Mbala Kisambi,Alphonce Temba aishauri Serikali kuhamasisha uwekezaji wa masoko mfano wa EACLC kote nchini

DAR-Mwenyekiti wa mradi mpya wa Mbala Kisambi uliopo mkoani Pwani,Alphonce Temba ameishauri Serikali kuangalia namna ya kufanikisha uanzishwaji wa masoko makubwa kote nchini ili kurahisisha biashara kwa wananchi na kukuza pato la Taifa.
Temba ameyasema hayo Machi 29,2025 baada ya kufanya ziara katika Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Temba amewashawishi wakurugenzi wa mradi huo kufungua soko kubwa zaidi eneo la Mbala ambako ni karibu na viwanda vingi katika Mkoa wa Pwani.

Amesema, EACLC ni miongoni mwa miradi mikubwa ambao unalenga kuboresha biashara na usafirishaji Afrika Mashariki, Kati na Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Temba amesema, uwekezaji huo ambao umefanyika katika kituo cha zamani cha Mabasi Ubungo umeipa Tanzania heshima kubwa, hivyo Serikali iendelee kuwaunga mkono na kuwakumbatia wawekezaji wenye maono mema kwa taifa.

"Wachina wameendelea kuwa watu wema kwa Taifa la Tanzania,hivyo wanapaswa kupewa heshima.Ni kwa kufungua soko la Kimataifa."

Kupitia soko hilo, Temba amesema, ameshuhudia hadhi yake huku likiwa la kisasa zaidi.

"Huu ni mfano wa kuiga Afrika Mashariki, ni soko ambalo wafanyabiashara wengi kukiwa na zaidi ya asilimia 50 ya wafanyabiashara wa Kariakoo na sehemu nyingine mbalimbali waliochukua fremu kwa kulipia kabisa kodi ya mwaka mzima.
Temba amesema, jengo la soko hilo linakidhi viwango vya ubora na limebeba hadhi ya kifahari.

Kupitia soko hilo, Temba amesema kuwa,ni mwanzo mzuri wa Serikali kuhakikisha masoko ya namna hiyo yanawekezwa kote nchini.

Ametoa mfano nchi ya Zambia ambayo ina idadi ndogo ya wananchi, lakini ina masoko mengi ya kisasa.

Temba amesema, masoko takribani sita yapo jijini Lusaka. Amesema, licha ya uwepo wa Soko la Kimataifa la Kariakoo ambalo linahudumia mataifa mbalimbali ya Afrika bado halijapangika ipasavyo.

Changamoto ya msongamano Kariakoo, Temba ameitaja kuwa moja ya kikwazo ambacho kimekuwa kikisababisha hasara na wakati mwingine wananchi huwa wanaibiwa huko.

Pia, ameeleza kuwa, kukosekana kwa mpangilio mzuri Kariakoo kumesababisha tafrani kubwa, kwani wengi wanapanga bidhaa chini, vyombo vya moto kukatiza kila mahali ikiwemo mikokoteni.

Anasema, hali hiyo imekuwa ikichangia mali nyingi kuwa katika hali ya uchafu hususani kipindi cha mvua.

"Lakini,soko hili (EACLC) limekuwa la Kimataifa kwa sababu limejengwa kwenye viwango vya juu.

"Mmoja wa wamiliki wa soko hili anadai kwamba,wafanyabiashara wengi katika eneo hilo watapata manufaa makubwa kwa sababu kutakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja kupitia wenye soko kwa viwanda vya China. Hivyo, kutumiwa mizigo na mali katika maduka yao kwa bei ya chini sana.

"Na jambo hili ninaloliona la wafanyabiashara wa Ubungo kwenye Soko la Kimataifa kupata link ya kupata mali kutoka kwenye viwanda vya China moja kwa moja utasaidia watu wengi waweze kufanya miamala yao kuagiza mizigo na kuja moja kwa moja pale kwenye maduka hayo kitu ambacho ni kizuri sana."

Vilevile ameeleza kuwa, soko hilo litasaidia kupunguza msongamano na vurugu Kariakoo ikiwemo ukwepaji wa kodi.

Amesema, namna soko hilo lilivyokaa litairahisishia Serikali kupata mapato yake ya ndani.

"Hususani kwa wafanyabiashara walioko ndani ya soko hilo."
Aidha, Mwenyekiti huyo amelipongeza soko hilo kwa kuweka mandhari nzuri ikiwemo kushiriki katika kuimarisha na kuinua uchumi wa Tanzania.

Mradi wa EACLC umejengwa katika eneo la zamani la stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani na una maduka na ofisi zaidi ya 2,000, ambapo wafanyabiashara wadogo na wakubwa, pamoja na watengenezaji wa bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania, China na nchi za Afrika Mashariki, watapata fursa ya kuuza na kununua bidhaa zao.

Aidha,kituo hicho ni cha kwanza kwa ukubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kupokea wafanyabiashara, na kinatarajiwa kuwa na mauzo ya dola milioni 500 kwa mwaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news