DAR-Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, akagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kiwanda cha uchapishaji cha Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ambao amesema ukikamilika utaifanya kampuni hiyo kujiendesha na kutoa huduma za uchapaji kwa taasisi nyingine.
Mhe. Mwinjuma amefanya ziara hiyo na kutoa kauli hiyo Machi 6, 2025 alipotembelea ofisi za TSN zilizopo eneo la Tazara, jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa kipaumbele cha Wizara ni kuhakikisha kiwanda hicho kinakamilika ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na kutokuwepo kwa kiwanda cha kujitegemea cha uchapaji.
“Naamini mradi huu utakapokamilika tutakuwa na TSN ya aina nyingine kabisa, inayoweza kujiendesha na kutoa huduma za uchapaji kwa taasisi nyingine zinazohitaji,” amesema Mhe. Mwinjuma.
Aidha Mhe. Mwinjuma amebainisha kuwa kwa sasa, TSN inachapisha magazeti yake mawili, yaani HabariLEO na Daily News, kwa kutumia vifaa vya taasisi binafsi, jambo ambalo amesema linatakiwa kufikia mwisho. “Kwa nguvu ambazo serikali imeweka mpaka sasa, jambo hilo litafanikiwa,” aliongeza.
Mhe Mwinjuma ameeleza kuwa ujenzi wa kiwanda hicho umefika asilimia 53.1, huku mitambo minne ikiwa tayari imeshafika na miwili ikiwa bado bandarini
“Nafahamu mbili zipo bandarini zikifanyiwa utaratibu wa kutolewa, na zitabaki zile ndogondogo kama 12 ambazo zitakamilisha mashine zote kwa asilimia 100,” amesema.
Mhe. Mwinjuma ameihakikishia TSN kuwa Wizara hiyo ina malengo ya kuwezesha kampuni hiyo kufanya kazi kwa urahisi na katika mazingira mazuri.
“Lengo ni kuwezesha taasisi hii si tu iweze kujiendesha, bali pia kuhudumu kwa Watanzania kwa kuwapa habari za kuaminika kutoka kwa taasisi inayoendeshwa na serikali,” amesema.
Pamoja na hayo Mhe. Mwinjuma aliwataka wafanyakazi wa TSN kufanya kazi kwa kuzingatia lengo la kuisemea serikali kwa kuwa kuna mambo mengi yaliyofanywa na serikali ambayo yanastahili kusemwa na kutetewa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Aisha Dachi, amesema kuwa kukamilika kwa kiwanda hicho kutaisaidia kampuni kuchapisha magazeti yake wenyewe na kufungua fursa za biashara kubwa zaidi.

Ameongeza kuwa lengo kuu ni kuboresha ufanyaji kazi na kufuata dira ya TSN ya kuwa daraja kati ya serikali na wananchi kwa kutoa habari za weledi.