LNA LUSUNGU HELELA
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amesema utashi wa kisiasa wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umeiwezesha TAKUKURU kupata vitendea kazi na kutimiza majukumu yake kwenye mazingira wezeshi.

Amesema, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita zaidi ya Watumishi 1000 wameajiriwa na TAKUKURU, ikiwa ni jitihada za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuiwezesha TAKUKURU.
Mhe.Sangu ametoa kauli hiyo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ilipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la TAKUKURU, Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Kamati hiyo kukagua miradi mbalimbali iliyotekelezwa na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora.
Amesema, mbali na magari 88 TAKUKURU iliyowezeshwa, inatarajia kwa mara nyingine tena kupokea jumla magari 100 ili kuwasaidia maafisa hao kutekeleza majukumu yao mahali popote na saa yeyote wanakohitajika.
Amesema hiyo ni nia ya dhati ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha TAKUKURU inakuwa na vitendea kazi vya kutosha na vya kisasa.
"Taasisi yetu sio tu inaziangalia Taasisi nyingine bali imekuwa mfano na kioo kwa Taasisi nyingine katika kuonesha thamani halisi ya fedha iliyotumika katika ujenzi wa jengo hili la Rombo," Mhe. Sangu amefafanua.
Katika hatua nyingine Mhe.Sangu ametoa pongezi kwa Kamati hiyo kwani ndiyo imekuwa ikifanya mambo yatokee, " mmekuwa mkipaza sauti kwa kufanya mapendekezo ya marekebisho ya bajeti kwenye miradi ya maendeleo kwenye Taasisi yetu ya TAKUKURU."