NA GODFREY NNKO
BENKI ya Biashara ya Taifa (NBC) imeingia makubaliano na Hope Holding Company Limited ambayo yatawezesha mteja kupata punguzo la asilimia 20 atakapofanya manunuzi kwa kutumia NBC Visa Debit Card katika maduka yao matano.

Makubaliano nayo yamefikiwa leo Machi 21,2025 katika jengo la Morocco Square jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia kuhusu ofa na makubaliano hayo, Mkuu wa Kitengo cha Miamala kutoka Benki ya NBC, Mangile Kibanda amesema, makubaliano hayo kati ya NBC na Hope Holding yatawezesha wateja kufanya manunuzi katika maduka yao matano ambayo yapo katika jengo hilo.
"Leo tupo hapa kwa ajili ya kusaini mkataba wa ushirikiano kati ya Benki ya NBC pamoja na wenzetu wa Kampuni ya Hope Holding kwa ajili ya matumizi ya kadi ambayo yatawezesha wateja wetu wa NBC ambao wana kadi zetu waweze kupata punguzo kupitia manunuzi watakayoyafanya katika maduka yao matano ambayo yapo katika jengo hili."
Amesema, wateja ambao wana kadi za NBC na wanafanya manunuzi katika maduka hayo wataweza kupata punguzo hilo kwa malipo ambayo watayafanya.
Amesema, wamefanya hivyo ikiwa ni muendelezo wa kampeni ambazo Benki ya NBC imekuwa ikizifanya hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu za Id El Fitr na Pasaka.
"Tunawaomba sana Watanzania ambao wana akaunti katika benki yetu kupita katika maduka haya na wakifika wasitembee na fedha taslimu, waje na kadi zao kwa ajili ya manunuzi ambayo watayafanya."
Amesema, ni kipindi ambacho wanawakaribisha wote kwa ajili ya kupata huduma na kununua zawadi kwa ajili ya watoto, ndugu, jamaa na marafiki.
Pia, amesema kwa wale ambao kadi zao zina changamoto waweze kufika katika matawi ya NBC ili kupata ufumbuzi kwa ajili ya kufanya malipo.
Wakati huo huo amewahimiza Watanzania ambao hawajawahi kufungua akaunti Benki ya NBC kufika katika tawi lolote kwa ajili ya kufungua akaunti.
Amesema, kupitia benki hiyo ni rahisi kwani unaweza kupakua app yao ya NBC Kiganjani na ukiwa na namba ya NIDA unaweza kufungua akaunti ambapo watakupatia kadi itakayokuwezesha kufanya malipo katika maduka hayo.
"Kwa hiyo, nikampeni ambayo tumeanza nayo leo na tutaendelea nayo mpaka kipindi cha Pasaka na Id El Fitr.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko kutoka Hope Holding, Mick Makame amesema, muunganiko huo ni hatua muhimu ambayo itawawezesha wateja kupata punguzo kubwa.
"Huu ni mwanzo, ninadhani kutakuwa na vitu vingine vizuri zaidi kwenye maduka yetu kupitia kadi ya NBC kuanzia hapa Morocco Square."