SINGIDA-Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeeleza nia yake ya kuwekeza zaidi kwenye maboresho ya viwanja vinavyotumiwa na vilabu mbalimbali nchini vinavyoshiriki Ligi Kuu ya NBC.

Benki hiyo ni moja ya wadhamini waliofanikisha ujenzi wa uwanja huo kupitia msaada wake wa fedha kiasi cha shilingi milioni 50 iliwakilishwa na maafisa wake waandamizi Elvis Ndunguru, Joseph Lyuba, Godwin Semunyu ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya ligi kuu ndani ya NBC, pamoja na maafisa wengine tawi la Singida.
Mkurugenzi wa Biashara wa NBC, Elvis Ndunguru amesema nia hiyo inakwenda sanjari na mikakati mingine ya benki hiyo katika kuboresha ligi hiyo ikiwemo utoaji wa mikopo ya usafiri kwa vilabu, utoaji wa huduma za bima ya afya kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi, usajili wa kadi za wanachama na utoaji wa elimu ya fedha kwa vilabu.

“Mbali na uwanja huu ambapo tuliwekeza kiasi cha sh milioni 50 tumeshasaidia viwanja vingine kwenye maboresho madogo madogo ukiwemo Uwanja wa Jamhuri Dodoma ambapo kupitia tawi letu la huko tulisaidia maboresho kwenye mfumo wa umwagiliaji wa uwanja,’’ amesema Ndunguru.
Ndunguru pia amevisisitiza vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo kuwekeza nguvu zaidi kwenye suala la utoaji wa kadi za kielectroniki kwa wanachama wake, hatua ambayo itavisaidia vilabu hivyo kujiongezea mapato na kutunza taarifa sahihi za wanachama wao.