Odinga akutana na Rais Salva Kiir kutathmini masuala ya kiusalama

JUBA-Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit leo Ijumaa ya Machi 28,2025 amekutana na Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Kenya,Raila Odinga, ambaye yupo nchini humo kwa misheni ya amani.
Raila amepewa jukumu na Jumuiya ya Nchi za Pembe ya Afrika (IGAD) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutathmini masuala ya kiusalama yanayoendelea Sudan Kusini, kwa lengo lililowekwa wazi la kuwezesha mazungumzo kati ya viongozi, ili kurejesha amani nchini humo.

Aidha,baada ya kuhitimisha kazi yake ya kutafuta ukweli huko Juba, Raila anatarajiwa kurejea na kutoa ripoti ya kina kuhusu hali ya sasa ya Sudan Kusini, huku eneo hilo likitoa wito wa mazungumzo.
Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa utulivu wa Sudan Kusini kwa eneo zima, wakitaja kuwa Sudan Kusini yenye amani, sio tu itaboresha usalama, lakini pia itaimarisha ushirikiano wa kikanda.

Haya yanajiri baada ya kuzuka hali ya sintofahamu,ni baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar kukamatwa na watu wenye silaha katika makazi yake yaliyopo Juba nchini humo.
Taarifa za kukamatwa kwa Machar zilianza kusambaa Machi 27, 2025 ambapo kukamatwa kwake kunahusishwa na mgogoro wa muda baina yake na Rais Salva Kiir.

Pia, ilidaiwa msafara wa magari 20 yaliyokuwa na silaha uliingia katika makazi ya Machar katika mji mkuu wa Juba na kumtia mbaroni.

Hata hivyo,kufuatia Sudan Kusini kupata uhuru mwaka 2011, Machar alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri huru ya Sudan Kusini huku Salva Kiir akiwa Rais.

Vita vilivyotokea kwa sababu ya mvutano wa kisiasa baina yake na Rais Kiir viliingiza nchi hiyo changa kabisa barani Afrika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Makubaliano ya amani kati ya Serikali ya Rais Kiir, mrengo wa Machar na wadau wengine ulifanyika 2018.Makubaliano hayo yalikuwa ndio msingi wa kuundwa kwa Serikali ya mpito nchini humo.

Februari 2020, Machar aliapishwa tena kama makamu wa kwanza wa rais kufuatia makubaliano hayo.

Machar ndiye kiongozi Sudan People's Liberation Movement-In Opposition-SPLM-IO) ikiwa ni kundi la mrengo wa upinzani kutoka chama tawala, ambao aliuanzisha mwaka 2014 kufuatia kuzuka kwa vita vya 2013.
Mgogoro wa hivi karibuni ulioripotiwa kwa wiki kadhaa katika nchi hiyo, umesababisha kuzorotesha hali ya usalama katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news