Pataneni na Russia

NA LWAGA MWAMBANDE

FEBRUARI 24,2022 inaendelea kubaki kuwa, tarehe yenye kumbukizi ya kuumiza na kuhuzunisha baada ya Urusi kuanzisha uvamizi mkubwa wa kijeshi dhidi ya Ukraine.
Picha na Skynews

Vita hiyo ambayo madhara yake yalionekana pia duniani kote, ilikuwa ni hatua ya kuendeleza mgogoro ulioanza mwaka 2014, baada ya Urusi kuchukua na kujiunga na eneo la Crimea kutoka kwa Ukraine.

Aidha,Urusi inadaiwa ilikuwa inatoa msaada kwa vikundi vya waasi Mashariki mwa Ukraine.

Miongoni mwa madhara ya vita kati ya Urusi na Ukraine ni vifo na majeruhi ambavyo vilijumuisha maelfu ya raia na wanajeshi.

Pia, yameshuhudiwa madhara makubwa ya uharibifu wa miundombinu mfano miji ya Kyiv, Mariupol na mingineyo huko Ukraine iliharibiwa vibaya, huku duniani ikishuhudia ongezeko kubwa la wakimbizi kutokana na vita hiyo.

Vita hiyo, kwa ujumla imeleta athari nyingi kwa pande zote mbili ikiwemo kiuchumi ambapo madhara yalivuka mipaka na kuleta mtikisiko mkubwa wa kiuchumi duniani.

Mbali na madhara ya kiuchumi, vita ya Ukraine na Urusi inatajwa kuleta athari hasi katika jamii na kisiasa ikiwemo mgawanyiko mkubwa na hofu kwa usalama duniani.

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema kuwa, sasa imetosha kwani wengi wanaumizwa na vita hiyo,hivyo ni wakati sahihi sasa Ukraine na Urusi kupatana. Endelea;

1. Wababe tanianeni, wenzenu tunaumia,
Na majina itaneni, huku sisi twafulia,
Vita vyenu komesheni, sisi tunaangamia,
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

2. Hadi sasa duniani, bado tunafikiria,
Hivi wapi ukingoni, vita vitapoishia,
Hasara takuwa nini, ile tutayoingia?
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

3. Hapa kwetu duniani, amani si kwa jambia,
Mkichomana mwilini, lazima mkatulia,
Mkiyajenga mezani, tamati weze fikia,
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

4. Vita kubwa duniani, kule zinakoishia,
Wala si kule vitani, hebu ndugu fwatilia,
Waliokuwa vitani, mezani wanaishia,
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

5. Kumbuka Ujerumani, walivyoishindilia,
Mwisho mwisho wa vitani, mezani walitulia,
Wakajadili mezani, itavyokuwa dunia,
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

6. Umoja wa Duniani, chanzo twakifahamia,
Waliokuwa vitani, mezani walitulia,
Wakaisaka amani, wasije kuangamia,
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

7. Vita vyote duniani, havijawahi sikia,
Vinacholeta uduni, roho zinaangamia,
Ikifikia mwishoni, kujenga mnarudia,
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

8. Tunachotaka amani, tusije tukaishia,
Maneno ya midomoni, si vema tunaumia,
Vikwazo vya redioni, mabomu yatuishia,
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

9. Majina yote iteni, hatutaki kusikia,
Mnatamba runingani, vipi mwatufikiria?
Bei bidhaa sokoni, sisi ndio twaumia,
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

10. Bei mafuta jamani, vita wanatutajia,
Bei zingine sokoni, nazo zitatupandia,
Kelele za mdomoni, ni wapi zitaishia?
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

11. Kakuzidi ulingoni, bora kusikilizia,
Ukijidai makini, watu wanaangamia,
Wewe uko hekaluni, t-sheti wajipigia,
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

12. Ulaya na Marekani, ya kwenu twayachukia,
Mwasogea Russia ndani, nini mnajitakia?
Mbona ya Cuba zamani, ulituchachamalia?
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

13. Ingekuwa ulingoni, Zelensky aingia,
Huku ang’atwe Putin, na kwa maumivu pia,
Tusingekuwa vitani, huku watuigizia,
Ukraine jamani, pataneni na Russia.

14. Russia yu kileleni, vile anajipigia,
Ukraine bondeni, vipigo vinaingia,
Bila kuwapo makini, dola itaangamia,
Ukraine jamani, pataneni na Russia,

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news