DAR-Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limefanikiwa kumnasua mtoto wa kiume wa miaka nane anayesoma Shule ya Msingi Mbezi katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mtoto huyo alitekwa Machi 6 , 2025 na Stanley Dismas Ulaya (18) mkazi wa Kata ya Nguruka katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Kamanda Jumanne Muliro amesema, Jeshi la Polisi Machi,8, 2025 lilimkamata kijana huyo na baadaye kumjeruhi kwa risasi alipojaribu kutoroka chini ya ulinzi na yuko Hospitali chini ya Jeshi la Polisi akipatiwa matibabu.
Amesema,mtuhumiwa huyo alitekeleza tukio hilo Machi 6, 2025 wakati mtoto huyo aliposhuka katika daladala kabla ya kuingia katika geti la shule ndipo alikamatwa na mtuhumiwa na kumpeleka hadi Bagamoyo mkoani Pwani.
Inadaiwa mtuhumiwa alikaa naye vichakani huku akitumia namba ya simu ya mzazi iliyokuwa kwenye madaftari kuipiga huku akidai pesa kwa vitisho ili amuachie na asimdhuru mtoto huyo na wasipotuma watakuta maiti.
Pia,Kamanda Muliro amebainisha kuwa, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam lilifanya kazi kubwa ya ziada ya ufuatiliaji na Machi 8, 2025 majira ya saa 01:00 usiku baada ya mtuhumiwa kukamatwa na kufikishwa kituo cha Polisi Oysterbay alijaribu kutoroka kwa kukimbia na kulazimika kumpiga risasi mguuni na kwenye paja
Jonson Elisha ambaye ni mzazi wa mtoto huyo amesema, yeye alimpeleka mtoto shuleni na kumuacha getini, lakini ilipofika jioni mtoto hakurejea nyumbani ndipo alipoanza kumtafuta na walimu wakamwambia kuna namba inawasumbua awasiliane nayo.
Amesema,alipoanza kuwasiliana nayo aliambiwa atume kiasi cha shilingi milioni 50 ndipo mtoto aachiliwe asipotuma atakuta maiti, hivyo akaamua kwenda kuripoti Kituo cha Polisi ili asaidiwe kwa hatua zaidi.
Wakati huo huo, Elisha amelishukuru Jeshi la Polisi kwa juhudi zao walizozifanya kuwasiliana na kwa mbinu zao na Machi 8, mwaka huu alipigiwa simu aende kituo cha Polisi kuchukua mtoto na alimkuta akiwa na afya njema.