PWANI-Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, amesisitiza umuhimu wa menejimenti na watendaji wakuu wa Wizara yake na wakuu Taasisi zilizo chini yake kujitambua na kuelewa jukumu lao kubwa katika kuwa "mtima, haiba, na taswira ya nchi."
Kauli hiyo ametoa Machi 17, 2025, wakati wa mkutano wa mafundo na mazingativu kwa viongozi wa Wizara hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Uongozi Mwl. Nyerere, Kibaha mkoani wa Pwani. Mhe. Kabudi amesisitiza kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ndio kiini cha utambulisho wa Taifa, hivyo ni wajibu wao kusimamia jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa.
"Sisi ni mtima wa Taifa, na jambo hili sio langu alilisema Mwl. Nyerere. Wizara hii ndio taswira ya nchi yetu. Mtu akitaka kujua nchi yetu inafananaje na ipoje, ni Wizara hii. Wizara hii ndio inaonyesha haiba ya Watanzania kwa maana ya mila zao, desturi zao, kucheka kwao, kulia kwao, kuimba kwao, kufurahi kwao, na kuhuzunika kwao," amesema Mhe. Prof Kabudi.
Aidha, Mhe. Kabudi aliwataka viongozi hao kujiuliza maswali muhimu kuhusu utambulisho wao na jukumu lao: "Je, sisi ni nani? Tunajitambua sisi wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, sisi ni nani? Nini dhima yetu? Nini wajibu wetu? Nini majukumu yetu? Lakini baada ya hapo, lazima tujiulize tunahitaji mbinu gani, mikakati gani ili huko kujitambua kwetu sasa kutimie,"Mhe. Prof Kabudi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Hamis Mwinjuma ameeleza kuwa lengo la kikao na mafundo hayo ni pamoja na kuongeza mshikamano miongoni mwa wafanyakazi wa Wizara na kupeana uelekeo hasa mahali walipotoka, walipo na wanapoelekea
“Imekuwa muhimu kwa sababu mara zote baada ya vikao hivi inafaamika kuwa morali ya kazi huwa inaongezeka hivyo upo muhimu wa kuwa na kikao hiki na sio mara moja kila mwaka hivyo tuendelee kukumbushana kuhusu wajibu ambao tunatazamiwa kuutekeleza katika majumu tuliyopangiwa lakini vilevile kupeana moyo na kurekebishana hata kupeana mwelekeo pale inapobidi,”amesema Mhe. Mwinjuma.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu na msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson msigwa, Naibu Katibu Mkuu, Methusela Ntonda watendaji wakuu wa wizara na taasisi.