ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa usimamizi thabiti wa uchumi wa Tanzania.
Dkt. Mwinyi alitoa pongezi hizo katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Madinat Al Bahr, Zanzibar.

“Naridhika sana na ushauri wa masuala ya uchumi tunaopewa na Benki Kuu na ndomaana uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla umekua vizuri huku tukiwa tunadhibiti mfumuko wa bei vyema,” alisema Dkt. Mwinyi.
Alihimiza ushirikiano endelevu kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki Kuu ya Tanzania ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanaimarika kwa manufaa ya wananchi wote.

“Zanzibar tuna utamaduni wa kusaidia jamii, hususani katika kipindi hichi cha ramadhani kwahiyo nashukuru sana na ninyi Benki Kuu mnao utaratibu huo, tunawapongeza sana,” alisema.
Kwa upande wake, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, alisema kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika, huku sekta ya fedha ikikua kwa kasi na mfumuko wa bei ukiwa chini ya wastani wa dunia.

“Kwa mwaka jana uchumi wetu umeendelea kukua, ambapo kwa Tanzania bara umekua wa asilimia 5.4 na Zanzibar asilimia 7, alisema.
Alibainisha kuwa Benki Kuu imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei, ambapo kwa mwaka 2024, Tanzania ilikuwa nchi ya tatu duniani kwa kuwa na mfumuko wa bei mdogo.
“Kwa Tanzania Bara, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.1, huku Zanzibar ukiwa asilimia 4.5, ikilinganishwa na mfumuko wa bei wa dunia wa asilimia 4.7,” alieleza.
Aidha, Gavana Tutuba alizungumzia changamoto katika huduma za kifedha na kuhimiza umuhimu wa elimu ya fedha kwa wananchi ili waweze kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya huduma za kifedha.
Benki Kuu imeandaa miongozo ya elimu ya fedha kwa watu walio katika mfumo rasmi wa elimu pamoja na wale walio nje ya mfumo rasmi, lengo likiwa ni kukuza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya fedha na kuimarisha ustawi wao wa kiuchumi.