ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amelishauri Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuisaidia Zanzibar kuendeleza Uchumi wa Buluu,kwani ni sekta muhimu kwa Uchumi na Ustawi wa wananchi wake.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipozungumza na Ujumbe wa Shirika hilo ukiongozwa na Mkurugenzi wake Mkuu Audrey Azoulay waliofika Ikulu Zanzibar tarehe 5 Machi 2025.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameuelezea ujumbe huo kuwa kwa sasa sekta ya Uchumi wa Buluu ndio kipaumbele cha Serikali inayohitaji kupewa msukumo wa ziada wa misaada ya kitaalamu,teknolojia na fedha ili kuwa endelevu na kuiwezesha nchi kunufaika na rasilimali za kutosha zilizomo baharini.
Amefahamisha kuwa,Uchumi wa Buluu una fursa nyingi zinazoweza kutoa mchango mkubwa wa maendeleo na ukuaji wa uchumi, fursa za ajira na kuimarisha maisha ya wananchi na kuishauri UNESCO kuwa tayari kushirikiana na Zanzibar kuendeleza sekta hiyo.
Rais Dkt.Mwinyi amesema,bado zipo changamoto nyingi katika kuuendeleza mji mkongwe ili ubaki katika haiba na urithi wake kutokana na kuwa na idadi kubwa ya nyumba zinazohitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa, Udhibiti wa Uingiaji na utokaji wa Magari unaopaswa kubadilika kulingana na Mazingira ya sasa ndani ya Mji Mkongwe bila kuathiri Maisha ya wakaazi wa Mji huo.
