DAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezihamasisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na Mifuko ya Maendeleo ya Petroli (Petroleum Fund) ambayo itasaidia katika utafiti, ubunifu, mafunzo na uendelezaji wa Sekta ya Mafuta kwa ujumla.

Ameeleza kuwa, Dira ya Afrika Mashariki ya 2050 inaelekeza kuhusu kuanzishwa kwa Mfuko huo wa Petroli hivyo huu ni wakati muafaka wa kutekeleza suala hilo kama lilivyoainishwa katika Ibara ya 114 ya Mkataba wa Afrika Mashariki ambayo inaelekeza kuimarisha mashirikiano katika kusimamia rasilimali kwa faida ya wote.

Rais Mwinyi pia ameeleza kuhusu umuhimu wa Rasimali za Mafuta na Gesi Asilia kuwa na mchango katika ukuaji wa Sekta nyinginezo akitolea mfano jinsi Sekta ya Mafuta nchini ilivyosaidia miradi ya umeme hasa usambazaji wa umeme vijijini.
Aidha, amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kujitolea kwake bila kuchoka katika maendeleo ya sekta zote ikiwemo mafuta na gesi ambapo chini ya uongozi wake miradi ya kimkakati katika Sekta hiyo imeendelea kutekelezwa.
Pia, amezipongeza Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufanya mkutano huo kwa mafanikio ikiwemo Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kamati ya kitaifa ya EAPCE 2025, Timu ya Kitaifa ya Uratibu na kamati zake ndogo.
