ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuijenga Zanzibar yenye Maendeleo Endelevu na huduma bora za jamii ikiwemo elimu, afya na maji safi na salama.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipoizindua Sera Mpya ya Maji na Usafi wa Mazingira ya 2025 katika hafla iliofanyika Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Wilaya ya Mjini.
Amesema, uzinduzi wa Sera ya Maji ni hatua muhimu ya kuyafikia maendeleo yanayotarajiwa na nchi katika uimarishaji wa huduma za upatikanaji wa maji na nyingine za kijamii.
Ameeleza kuwa, Sera Hiyo Mpya ya 2025 itaimarisha usimamizi wa rasilimali maji na itahakikisha huduma za upatikanaji wa maji kwa kila mwananchi, kusaidia kupunguza athari za tabia nchi zinazotokana na uchafuzi wa mazingira.
Amebainisha kuwa, sera hiyo pia itaimarisha elimu kwa umma juu ya usimamizi wa mazingira,mifumo ya usimamizi wa maji taka na kuimarisha uwekezaji katika miundombinu ya maji pamoja na ushirikiano wa wadau, Sekta Binafsi na Sekta ya Umma.
Dkt.Mwinyi amewahakikishia wadau na wananchi kuwa, Serikali itaendelea kuweka miundombinu ili miji na vijiji vilivyo mbali na miji vipate maji safi na salama.
Ameeleza kuwa, hatua hiyo itaenda sambamba na kuwashirikisha wadau na Sekta Binafsi kwa kuifuata Miongozo ya Sera hiyo mpya Ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa na uhakika wa maji safi na salama.

Amesema kuwa,uandaaji wa sera hiyo ni utekelezaji wa shughuli zilizoainishwa katika Mpango wa Utekelezaji wa Sekta ya Maji wa 2022 hadi 2027.
Rais Dkt.Mwinyi ameipongeza Wizara ya Maji, Nishati na Madini kwa kutekeleza mpango huo kwa ufanisi aliouelezea kuwa na tija kwa nchi.
Ameeleza kuwa, sera hiyo pia itaimarisha usimamizi wa rasilimali maji na kuhakikisha upatikanaji wa maji Unguja na Pemba pamoja na usimamizi wa maji taka kwa kuhakikisha mazingira yanatunzwa ipasavyo.