TANGA-Ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imewekeza zaidi ya trilioni 6 kwenye mamlaka za serikali za mitaa kote nchini.

Hayo yamesemwa Ijumaa Februari 28, 2025 katika uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga na Kaimu Waziri wa TAMISEMI Mhe Deogratius Ndejembi ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Sambamba na hilo, Ndejembi amesema, Serikali imetoa kibali cha kuajiri zaidi ya watumishi wa kada ya afya 25,900 ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Ameongeza kwa kusema kuwa, katika sekta ya elimu, Serikali ya Rais Samia imetenga na kutoa shilingi trilioni 3.98, ambazo zimechangia ujenzi wa shule mpya za msingi zaidi ya 468, vyumba vya madarasa zaidi ya 12,452 vya shule za msingi, na shule za awali zaidi ya 1,600 ambazo hazikuwepo kabla.
"Kupitia fedha hizo, shule za sekondari za kata zaidi ya 704 zimejengwa, huku vyumba vya madarasa zaidi ya 41,000 vikiwa vimejengwa katika shule za sekondari. Pia, zaidi ya mabweni 1,600 yamejengwa ili kupunguza umbali wa wanafunzi wanaotembea kufuata elimu,"alisema Ndejembi.
Kuhusu miundombinu ya barabara, amesema Serikali imeongeza bajeti ya TARURA kutoka bilioni 654 hadi trilioni 1.59, ambapo Mkoa wa Tanga umenufaika kwa ongezeko la bajeti kutoka bilioni 12 hadi bilioni 34 kwa mwaka.
Kupitia bajeti hiyo, zaidi ya kilometa 819 za barabara za lami zimejengwa nchini, zikiwemo barabara za Tanga Mjini kutoka barabara ya kwanza hadi ya 21. Barabara za changarawe zimejengwa kwa zaidi ya kilometa 11,900 kote nchini.
"Rais Samia ameendelea kuwekeza katika masoko na maeneo ya biashara, ambapo hivi karibuni Serikali anayoiongoza imetoa zaidi ya bilioni 36.6 kwa ajili ya ujenzi wa soko la Makorora, pamoja na soko la kisasa la samaki. Pia, mwambao wa Raskazone utafanyiwa maboresho kwa kilometa nne ili kuimarisha mandhari na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo,"alisisitiza.
Waziri Ndejembi amesisitiza kuwa kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia inaendelea kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi, huku akiwahimiza wakazi wa Tanga kuendelea kumuunga mkono katika juhudi zake za kuleta maendeleo nchini.