DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kuilinda misingi inayoiongoza sekta ya ardhi.
Lengo ni kuhakikisha kuwa,Watanzania wananufaika na rasilimali hiyo, na amesisitiza kuwa ardhi yote ni mali ya umma wa Tanzania.


Aidha, Rais Dkt. Samia amewataka watumishi kwenye sekta ya ardhi kubadilika na kufanya kazi kwa weledi na kwa haki na amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi kuchukua hatua stahiki kuwawajibisha watumishi wote wanaokwamisha utendaji wa Wizara hiyo.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesema kuwa Sera ya Ardhi iliyoboreshwa imeweka sharti la kuwataka wamiliki kusajili ardhi zao na ili kuimarisha usalama wa milki, Serikali inataka kila kipande cha ardhi nchini kipangwe, kipimwe na kisajiliwe.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa ili kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya milki hususan makazi ya bei nafuu, Sera iliyoboreshwa inaweka utaratibu wa kuwezesha waendelezaji milki wa kigeni kuwekeza katika sekta ya nyumba na kuuza kwa wenye uhitaji.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amesema kupitia Sera hiyo Serikali inaenda kuchochea ushirikishwaji zaidi wa sekta binafsi katika sekta ya milki, hususan ujenzi wa makazi ya bei nafuu maeneo ya mijini na vijijini, hatua inayolenga pia kuimarisha uwezo wa wananchi wote na hasa vijana wanaoanza maisha kupata makazi kwa bei nafuu.