ZANZIBAR-Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano mkuu wa Kimataifa wa Shirikisho la Vyama vya Mawakala wa Ushuru na Forodha unaotarajiwa kufanyika Aprili 30 hadi Mei 1, mwaka huu katika Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari Waziri wa Uchukuzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Makame Mnyaa Mbarawa katika Ukumbi wa Mikutano katika Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema Mkutano huo utashirikisha washiriki zaidi ya 500 kutoka nchi za Kimataifa kwa upande Afrika na Mashariki ya kati wakiwemo wataalamu wa usafirishaji wa lojistiki, watunga sera, wataalamu wa uwezeshaji biashara, mamlaka za udhibiti, mamlaka za bandari, wasafirishaji mizigo, watafiti na wabunifu wa sekta hizo Duniani.
Amesema lengo la Mkutano huo kubadilishana maarifa kwa kufanya majadiliano juu ya mbinu bora na utafiti wa kisasa kuhusu vifaa endelevu vya kutumia teknolojia ya kisasa pamoja na kukuza ushirikiano wa kati ya watoa huduma za vifaa, mamlaka za udhibiti wa uzalishaji, wauzaji wa rejereje na kampuni za teknolojia.
Aidha ameeleza kuwa mkutano huo utajadili mstakabali wa kuchunguza mageuzi ya kidigitali, teknolojia mpya na suluhisho za ubunifu katika sekta ya vifaa (logistic) ili kupunguza athari za mazingira.
Waziri Mbarawa amesema pia kutakuwa majadiliano kuhusu sera ya kukuza mazingira kisheria yanayounga mkono sekta bora na kuweka vifaa endelevu pamoja na kutoa jukwaa la washiriki kuungana na wateja, wawekezaji na washirika wapya ili kuimarisha ujuzi na ushindani katika sekta ya vifaa na usafirishaji.
Sambamba na hayo amefahamisha kuwa Mkutano huo utazungumzia maswala ya urahisishaji biashara, ufadhili, bima, teknolojia na uboreshaji wa taaluma ndani ya tasnia ya usafirishaji na lojistiki ili kupata nafasi ya kufahamu fursa zinazotokana na mpango wa eneo huru la biashara Afrika pamoja na mchango wa tasnia ya hiyo katika kusaidia ukuaji wa uchumi endelevu barani Afrika, Mashariki ya kati na Ulimwenguni.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Makame Machano Haji amevipongeza vyama vya ushuru na forodha kwa jitihada na mafanikio kwa kuitetea fursa ya kuifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Vyama vya Mawakala wa Ushuru na Forodha kwa upande Afrika na Mashariki ya kati.
Ameeleza kuwa, Serkali imejipanga kuwapokea washiriki wote wa Mkutano huo na kuwahakikishia kwamba kutakuwa amani na utulivu pamoja na kupata fursa ya kutembelea maeneo ya utalii yaliopo nchini.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Mawakala wa Ushuru na Forodha Tanzania Edward Urio ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo nchini na kuahidi kutoa ushirikiano katika kipindi chote cha mkutano utakapokuwa unaendeleo.
Katika mkutano huo shughuli mbali mbali zitafanyika ikiwemo maonesho ya bidhaa na huduma ambapo kauli mbiu ni “Ushirikiano katika Uchumi wa Buluu kubadilisha lojisiki na uchukuzi kwa uendelevu”