DAR-Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace amejibu tuhuma wanazoshushiwa bodi ya Ligi kufuatia uamuzi wa kuahirisha mchezo wa Kariakoo Derby uliopaswa kuchezwa Machi 8, 2025.
Akizungumza katika mahojiano na Wasafi Fm katika kipindi cha Jana na Leo, Rais Karia amedai kuwa bodi iachwe ifanye kazi yake.
Pia,amebainisha kuwa,walisimamia na watasimamia kanuni na sheria inavyopaswa, lakini kwa wanaosema bodi hiyo itenguliwe nao wanapaswa kujihoji kama uongozi wao upo sawa.
"Taratibu tuziache zifuatwe, Lakini huwezi kusema bodi ijiuzulu. Hata wanaosema wawaambie na viongozi wao, hawastahili kujiuzulu?.
"Vitu vingine vinafanyika kitoto,kama watu wamechoka kucheza mpira basi wakaendelee na sinema zao.
Mbali na hayo amesema kuwa, “Kuna siku tulipokea barua kutoka CAF wakihitaji waamuzi wetu wawili kwenda kuchezesha michuano ya Kimataifa.
“Wakati barua ile imekuja ofisini kuhitaji wale waamuzi kulikuwa na changamoto. Kwani mojawapo ya wale waamuzi ambaye ni Ahmed Arajiga alikuwa amefungiwa na kamati ya masaa 72.
“Ilikuwa ngumu sana kwangu, maana CAF wamemtaka mwamuzi, halafu huku kwetu kamati imemfungia, lakini nikafanya maamuzi.
“Nilifanya maamuzi nikawaambia hawa waamuzi waruhusiwe waende,walienda wote wawili,lakini bahati mbaya mmoja ndio alifuzu ambaye ni Ahmed Arajiga.
“Yalikuwa maamuzi magumu ila sikuwa na namna na Ahmed Arajiga alienda kuwakilisha Tanzania vema sana.Hata mechi aliyochezesha alichezesha vizuri sana”