MARA-Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo tarehe 11 Machi, 2025 ameongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji na kuwataka wajumbe wa kikao hicho kuwa mabalozi ya mambo yote yaliyojadiliwa katika kikao hicho.

Aidha, Bwana Kusaya ameahidi kufuatilia taarifa ya baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Mkoa wa Mara kutokufanya vikao vya mabaraza ya wafanyakazi kwa muda mrefu na kuchukua hatua pale ambapo mabaraza hayo hayajafanyika kutokana na uzembe.
“Hivi ni vikao vya kisheria, ni lazima vifanyike kwa mujibu wa Sheria na taratibu na wajumbe walipwe posho zilizoainishwa kwenye miongozo ya Serikali na kama wanakopwa lazima wajue kuwa wamekopwa” amesema Bwana Kusaya. 

Bwana Kusaya amewashukuru viongozi wa TUGHE Mkoa wa Mara na wajumbe wa kikao hicho walioshiriki na kutoa michango yao na kuwataka kuhakikisha michango wanaoitoa katika vikao hivi iwakilishe mawazo na maoni ya wafanyakazi waliowachagua kuwawakilisha.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Bwana Emmanuel Mazengo amesema Sekretarieti ya Mkoa katika mwaka wa fedha 2025/2026 inatarajia kutumia jumlya ya shilingi 10,708,542,000.00 kwa ajili ya kulipa mishahara, matumizi mengineyo na kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Kati ya fedha zote zitakazotumika mishahara ni shilingi 2,989,988,000.00, matumizi mengineyo ni shilingi 4,395,388,000.00 wakati miradi ya maendeleo ikitengewa shilingi 3,323,166,000.00,” amesema Bwana Mazengo.
Bwana Mazengo amesema fedha za maendeleo ziatarajia kutekeleza miradi ya ukamilishaji wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, ujenzi wa nyumba ya kupumzikia viongozi, ukarabati wa nyumba ya Mkuu wa Mkoa na miradi ya kujitegemea.
Bwana Mazengo amesema miradi mingine ya maendeleo iliyotengewa fedha katika bajeti hiyo ni usimamizi wa mitihani, ununuzi wa gari moja la kiongozi na ufuatiliaji na tathmini.
Bwana Mazengo amesema vipaumbele vya bajeti ya Sekretarieti ya Mkoa ni kusimamia na kudumisha masuala ya usalama, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapiduzi ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa.
Aidha, Bwana Mazengo ameahidi kuwa kama ukomo wa bajeti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara utaongezwa, Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Sehemu na Vitengo pia zitaongezewa bajeti ili kupunguza nakisi ya bajeti katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Mara Bwana John Boman amesema kuna baadhi ya Halmashauri ambazo hazifanyi vikao vya mabaraza ya wafanyakazi na haviruhusu majadiliano na watumishi katika masuala ya msingi ya Halmashauri hizo.
Bwana Boman ameitaka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara kuendelea kutoa elimu kwa watumishi kuhusu ujazaji wa taarifa za utendaji wao katika mfumo wa PEPMIS ili wafanyakazi wasipate vikwazo vya kutolipwa mshahara na kukataliwa kupandishwa vyeo na hatimaye kuathiri pensheni za watumishi hao.
Pamoja na mambo mengine, kikao cha baraza la wafanyakazi kimejadili ajenda kuu moja Mpango wa Bajeti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo wajumbe wametoa mapendekezo mbalimbali ya kuboresha bajeti hiyo.
Kikao cha Baraza la Wafanyakazi kimehudhuriwa na Wakuu wa Sehemu na Vitengo wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya za Mkoa wa Mara na wawakilishi mbalimbali kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.