NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ),Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kwa njia ya mtandao pamoja na viongozi mbalimbali akiwa Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika mkutano huo ambao umefanyika Machi 13,2025 umefunguliwa rasmi na kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mheshimiwa Dkt. Emmerson Dambudzo Mnangagwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa SADC.
Viongozi wa nchi na Serikali, na wawakilishi walioudhuria mkutano huo walijadili hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mbali na Rais Dkt.Samia na Dkt.Mnangagwa, wengine walioshiriki ni Rais wa Jamhuri ya Botswana,Wakili Duma Gideon Boko, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mheshimiwa Rais Mr. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo.
Wengine ni Rais wa Madagascar,Mheshimiwa Andry Rajoelina, Rais wa Msumbiji: Mheshimiwa Daniel Francisco Chapo, Rais wa Namibia, Mheshimiwa Dkt.Nangolo Mbumba, Rais wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Cyril Matamela Ramaphosa na Rais wa Zambia, Mheshimiwa Hakainde Hichilema
Kwa upande wa Lesotho, mwakilishi alikuwa ni Mheshimiwa Waziri Mkuu,Ntsokoane Samuel Matekane, Eswatini ni Mheshimiwa Waziri Mkuu Russel Dlamini na Malawi ni Mheshimiwa, Bi.Nancy Gladys Tembo, Waziri wa Mambo ya Nje.
Aidha,Mauritius iliwakilishwa na Mheshimiwa Dhananjay Ramful, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Biashara ya Kimataifa, Angola ni Manuel Homem, Waziri wa Mambo ya Ndani huku Seychelles ikiwakilishwa na Mheshimiwa Claude Morel ambaye ni Balozi nchini Afrika Kusini.
Mkutano huo ulipokea taarifa za hivi karibuni kuhusu hali ya usalama katika Mashariki mwa DRC na kujadili Ripoti ya Misheni ya Walinda Amani wa SADC nchini DRC (SAMIDRC) kutoka mkutano wa SADC Organ Troika uliofanyika Machi 6,2025.
Vilevile,mkutano ulitoa pole kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jamhuri za Afrika Kusini, Malawi na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na familia za wanajeshi waliopoteza maisha wakiwa katika operesheni za SAMIDRC, na kuwatakia waliojeruhiwa uponyaji wa haraka.
Aidha,mkutano huo ulieleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya usalama inayozidi kuzorota Mashariki ya DRC, ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa kwa miji ya Goma na Bukavu, na kuzuiliwa kwa njia kuu za usambazaji mahitaji, hali ambayo imeathiri usafirishaji wa misaada ya kibinadamu.
Katika hatua nyingine,mkutano huo ulipongeza vikosi vya kijeshi kwa kujitolea,umoja na juhudi zao thabiti tangu kuanza kwa operesheni.
Mkutano ulitoa wito wa kulinda na kuruhusu kwa uhuru raia wanaotafuta usalama, na kuhimiza pande zote kuheshimu kanuni za kimataifa za kibinadamu, kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya raia, na kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bila vizuizi.
Kupitia mkutano huo, viongozi hao walizingatia ongezeko la mahitaji ya kibinadamu nchini DRC na kuitaka jumuiya ya Kimataifa ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kutoa msaada wa kibinadamu kwa wananchi wa DRC.
Mkutano ulisitisha dhamana ya SAMIDRC na kuagiza kuanza kwa mchakato wa kuondoa vikosi vya SAMIDRC kutoka DRC kwa awamu.
Pia,mkutano ulisisitiza kujitolea kwao kutatua mgogoro unaoendelea nchini DRC na kuimarisha juhudi za kuleta amani ya kudumu na usalama katika Mashariki mwa DRC, kulingana na Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa SADC wa mwaka 2003.
Mkutano ulisisitiza kujitolea bila kutetereka kuendelea kusaidia DRC katika kulinda uhuru,mshikamano na umoja wake nchini humo pamoja na amani endelevu, usalama, na maendeleo.
Mkutano huo ulirudia haja ya kupata suluhisho la kisiasa na kidiplomasia kwa kushirikiana na pande zote ikiwa ni pamoja na pande za serikali, zisizo za serikali, kijeshi katika Mashariki mwa DRC ili kurejesha amani, usalama na utulivu nchini humo.
Wakati huo huo,mkutano huo ulirudia pia uamuzi kutoka kwa Mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC wa kuunganishwa kwa mchakato wa Luanda na Nairobi na kuongezewa kwa wawezeshaji zaidi ili kuimarisha mchakato wa kujenga amani.
Mkutano ulikaribisha Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) 2773 ambalo linatoa miongozo kwa suluhisho la kudumu huku likiunga mkono juhudi za kanda za Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (ECCAS),
Mkutano wa Kimataifa wa Nchi za Mikoa ya Maziwa Makuu (ICGLR), na SADC, katika kuandaa mikutano ya ngazi ya juu na juhudi za chini ya michakato ya upatanishi ya Luanda na Nairobi, pamoja na juhudi za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kurejesha amani na usalama Mashariki mwa DRC.
Mkutano ulitambua shukrani zilizotolewa na Mheshimiwa Rais Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo wa DRC kwa msaada wa SADC katika kushughulikia changamoto za kiusalama zinazokabiliana na DRC.
Aidha,mkutano ulimpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mwenyekiti wa Organ ya SADC, kwa uongozi wake thabiti katika kushughulikia masuala ya amani na usalama katika kanda ya SADC.
Pia,mkutano huo ulimshukuru Mwenyekiti wa SADC, Mheshimiwa Dkt. Emmerson Dambudzo Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, kwa kuitisha mkutano huo wa SADC na kwa uongozi wake katika kukuza ushirikiano wa kanda kuelekea kufikia amani, usalama na utulivu katika kanda hiyo.
Naye Mwenyekiti wa SADC alieleza shukrani zake kwa viongozi wa nchi na Serikali kwa kuhudhuria mkutano huo kwa njia ya mtandao na kwa kujitolea kwao kushirikiana katika ajenda za kikanda.