NA LWAGA MWAMBANDE
REJEA katika Biblia Takatifu kitabu cha Ruthu 1:15-16, neno la Mungu linasema, ¹⁵Naye akasema,tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako.
¹⁶Naye Ruthu akasema,usinisihi nikuache, nirejee nisifuatane nawe; maana wewe uendako nitakwenda, na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu."
Ukilitafakari neno la Mungu katika hii mistari utaona wazi kuwa,miungu (mungu) ya Wamoabu ilikuwa ya uongo,lakini Mungu aliyekuwa anamtukia Naomi ambaye ni Mbethlehemu alikuwa ndio Mungu wa kweli.
Yohana 3:16 inamthibitisha Mungu huyo wa kweli kwa kusema kuwa, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele."
Tunaona ingawa Naomi alikuwa yuko nchi ya Wamoabu,lakini wakati anarudi nchi yake,njiani alikuwa anarudi na wakwe zake wawili yaani Ruthu na Orpa.
Orpa aliishia njiani, hakuambatana na Naomi, lakini Ruthu aliambatana na Naomi japokuwa Naomi alimlazimisha kurudi,lakini yeye Ruthu alionyesha msimamo.
Ukiisoma Biblia kwa kina utaona inatukumbusha Wakristo wa leo tusiwe kama Orpa, kumuacha Yesu na kuyarudia ya dunia, kwani ukifanya hivyo ndio unakwenda kuangamia kabisa.
Kwa msingi huo,ukiamua kumfuata Yesu Kristo hakikisha umejikana nafsi na unamfuata ni bila kujali unapitia dhiki gani,au unapitia wakati gani mgumu.
Tumeona, Ruthu hakuangalia madhaifu alivyokuwa nayo Naomi kwamba atakuwa anatukanwa au la! aliamua kumfuata.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema tukirudi nyuma kama Orpa itakuwa tunajitafutia kuangamizwa zaidi,yafaa ukianza safari usirudi nyuma. Endelea;
1:Upendo wa Ruthu huu, kwa kweli ni wa pekee,
Alivyomuweka juu, mama mkwe atetee,
Alosema ni makuu, imani atuchochee,
Ukiianza safari, si vema kurudi nyuma.
2:Huyu alikuwa binti, ngoja nimuelezee,
Mtu mzima si denti, hadi ndoa itokee,
Hakuzaa hata senti, vile mume apotee,
Ukiianza safari, si vema kurudi nyuma.
3:Na mwanamke mwenzake, kidogo nimwelezee,
Wote walikuwa wake, kwa waume wapotee,
Mwenzake libaki zake, mamkwe apotezee,
Ukiianza safari, si vema kurudi nyuma.
4:Ila Ruthu kuolewa, liona aendelee,
Japokuwa alifiwa, na mume akiwa chee,
Wala hakujaribiwa, kwamba asiendelee,
Ukiianza safari, si vema kurudi nyuma.
5:Naomi liwashawishi, naye wasiendelee,
Uwe wa kwao utashi, kizazi kisipotee,
Wabaki wawe wapishi, na ndoa ziendelee,
Ukiianza safari, si vema kurudi nyuma.
6:Mmoja aliamua, naye asiendelee,
Ruthu yeye liamua, na mkwe aendelee,
Alichukua hatua, akitaka sipoteee,
Ukiianza safari, si vema kurudi nyuma.
7:Uendako nitakwenda, Ruthu na aendelee,
Mungu wako tampenda, barakaze nipokee,
Liazimu kutopinda, watu awapendelee,
Ukiianza safari, si vema kurudi nyuma.
8:Mungu tunapomwamini, hili funzo tupokee,
Hapo tuile yamini, mbele na tuendelee,
Kigeugeu uhuni, kwetu usitutokee,
Ukiianza safari, si vema kurudi nyuma.
9:Tumeacha ya dunia, ya Mungu tuendelee,
Huko tuiweke nia, na imani tuchochee,
Hadi mwisho wa dunia, kumlaki tupepee,
Ukiianza safari, si vema kurudi nyuma.
10:Mungu akusaidie, ya Ruthu uyapokee,
Na wewe uyatumie, na mbele uendelee,
Kwake Mungu utulie, na wala usipotee,
Ukiianza safari, si vema kurudi nyuma.
(Ruthu 1:8-18)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
@_Moto Ulao Online Church