Salamu za Jumapili: USIMDHARAU MTU

NA LWAGA MWAMBANDE

KATIKA nyakati za sasa,kuna watu tumekuwa tukijiona kuwa ni bora kuliko wengine katika jamii, maeneo mbalimbali au sehemu zinapotupatia riziki.
Pengine bila kutambua kuwa,kujiona kuwa ni bora kuliko wengine ni kujihesabia haki.

Ifahamike kuwa,Mungu humshusha mtu anayejiona kuwa ni bora kuliko wengine, tena huwashusha hata motoni kwa sababu dharau ni dhambi.

Rejea Biblia Takatifu kitabu cha 1 Wathesalonike 5:14 neno la Mungu linasema, "watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote.”

Tunapaswa kuwatia moyo wale tunaoona ni dhaifu, duni wala hawawezi kuliko kuwasema na kuwadharau bure popote ulipo.

Pia, rejea Wafilipi 2:3-5... “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.

...4 》Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.

...5》Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu.”

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,katika maisha yako usithubutu kumdharau mtu yeyote. Endelea;

1.Usimdharau mtu, hata asiye elimu,
Usimdharaau mtu, hata wa pesa adimu,
Mungu huyu ndiye wetu, ni wa haki anadumu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

2. Hata kama ni tajiri, miguu miwili dumu,
Huna wote ufahari, mwanadamu unadumu,
Uwe na tabia nzuri, kwa Mungu utahitimu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

3. Kule huyo asi kitu, pengine ni mhudumu,
Sote huyu Mungu wetu, aweza kumpa zamu,
Kujikusanyia vitu, maisha yawe matamu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

4. Kama kupindua meza, Mungu hivyo anadumu,
Walokuwa wanaweza, na wakakosa nidhamu,
Pazuri awafukuza, wawe maisha magumu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

5. Kumbuka Nebukadreza, alivyokuwa mtamu,
Mkuu lijieneza, dunia limfahamu,
Kwa kule kujitukuza, akaupata wazimu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

6. Litupwa huko porini, kama ni mwendawazimu,
Toka juu kawa chini, kama mbingu na kuzimu,
Ndiye Mungu wa mbinguni, alifanya tufahamu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

7. Mwangalie na Yusufu, alipita njia ngumu,
Ndugu walimkashifu, wamuuze pesa tamu,
Katangazwa kama mfu, kwa nguo kujazwa damu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

8. Hakuuzwa mara moja, kuuzwauzwa lidumu,
Kufika kwa nyumba moja, wakapata ufahamu,
Baraka nyingi si moja, ziliwafika kwa zamu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

9. Lakini mwovu ni mwovu, huko nako hakudumu,
Mke akaleta mbivu, aweze kumhudumu,
Yusufu macho makavu, kukubali kala ngumu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

10. Matokeo ya ukweli, wala kwake si ya hamu,
Mke akamkabili, kubaka kimtuhumu,
Na akafanywa dhalili, kule jela akadumu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

11. Mungu wa ajabu sana, kumwamini vema dumu,
Likuwa naye kijana, licha hali ile ngumu,
Vile alivyopambana, tiki zilizidi dumu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

12. Aliyekuwa mtumwa, kwa mtu akihudumu,
Mara watu wakatumwa, fursa imekwishatimu,
Nguo mpya zikafumwa, aende akahudumu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

13. Kaenda hadi ikulu, kwenda toa ufahamu,
Yeye akawa ni lulu, kwa ile yake elimu,
Kwa Farao kafaulu, usaili wa muhimu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

14. Mtumwa tena mfungwa, mgeni twamfahamu,
Naye Mungu akajengwa, kushika kazi muhimu,
Wala hakuwa na nongwa, ndugu walomhujumu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

15. Yule walimdharau, ndoto zake akidumu,
Wazijue angalau, lomuona kichwa ngumu,
Huko akapanda dau, bila wao ufahamu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

16. Yeye aliwatambua, bila wao kufahamu,
Wala hakuwasumbua, vile aliwahudumu,
Hapa hoja aibua, ambayo kwetu muhimu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

17. Usimdharau mtu, hata kama ala ndumu,
Mungu wake Mungu wetu, aweza kumhudumu,
Ageuke awe kwatu, kufanya mema adumu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

18. Kesho kikutana naye, bosi wewe mhudumu,
Vipi endapo na yeye, akikuwekea ngumu,
Mungu wetu huyu ndiye, anatupa ufahamu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

19. Vipi Daudi kijana, ikulu alohudumu,
Goliathi kapigana, licha ndugu mtuhumu,
Mara ndiye twamuona, apakwa mafuta humu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

20. Na hata akina Petro, watu waso na elimu,
Waloonekana ziro, kwenye ufahamu,
Kwake Yesu siyo kero, vema walivyohudumu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

21. Hata mwenzangu ulivyo, na wako ubinadamu,
Usijione wa hovyo, jinsi hali livyo ngumu,
Ndivyo Muweza alivyo, kutupenda anadumu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

22. Zidi kumtegemea, sala sadaka zidumu,
Aweze kutembelea, muda usiofahamu,
Mema kutokelezea, nawe utese kwa zamu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.

23. Wanadamu kawaumba, hao wote waheshimu,
Usiwaone washamba, unapokula vitamu,
Asijekufunga kamba, akakusweka kuzimu,
Aweza fanya chochote, aso mtu awe mtu.
(Mwanzo 41:9-44, 45:1-9, Danieli 4:1-35)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news