Salamu za Jumapili:LAZIMA LIPA GHARAMA-2

NA LWAGA MWAMBANDE

ZINGATIA kuwa,kumtumikia Mungu kuna faida nyingi zaidi maishani mwako, faida ambazo zinaanzia rohoni hadi mwilini ikiwemo heshima ambayo hauwezi kuipata popote pale duniani.
Rejea, Yohana 12:26 neno la Mungu linasema, ''Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba (MUNGU) atamheshimu."

Lakini, ili uweze kujiungamanisha na Mungu kikamilifu kuna gharama mbalimbali ambazo unapaswa kulipa. Miongoni mwa gharama hizo ni kuhakikisha unajitoa kulisoma neno la Mungu na kuomba,kujitoa kwa ajili ya kumtumikia Mungu, kuwa Mtakatifu na msafi.

Ukitafakari neno la Mungu utapata majibu ikiwemo kitabu cha Matendo ya Mitume 6:4 “na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.”

Vilevile,Wakolosai 4:12 neno la Mungu linaeleza kuwa,“Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu.”

...1 Yohana 2:1 neno la Mungu linasema, “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki."

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anaendelea kusisitiza kuwa, yafaa kupoteza yote duniani ili uyapate ya mbinguni. Endelea;

1:Mungu ukimfuata, lazima lipa gharama,
Siyo wampatapata, kirahisi ninasema,
Funzo kwa Ruthu twapata, jinsi alivyochagama,
Poteza ya duniani, uyapate ya mbinguni.

2:Ruthu wake Umoabi, kama Neno tukisoma,
Liwaacha kinabibi, wajomba kaka na mama,
Kuambatana na Rabi, Mungu wetu huyu wema,
Poteza ya duniani, uyapate ya mbinguni.

3:Kwa mume alikufa, bila kukizaa chema,
Huo ulikuwa ufa, angebaki alal
Lakini kwa maarifa, kubaki homu ligoma,
Poteza ya duniani, uyapate ya mbinguni.

4:Mama mkwe kuondoka, na yeye neno kasema,
Ya kwamba ataondoka, wala hatabaki nyuma,
Kwa Naomi amefika, wala kwao hatakwama,
Poteza ya duniani, uyapate ya mbinguni.

5:Wale wote ndugu zake, wote liwaacha nyuma,
Mila tamaduni zake, kama mate lizitema,
Kabeba za mkwe wake, tena mzimamzima,
Poteza ya duniani, uyapate ya mbinguni.

6:Kitu tunachojifunza, kumwamini Mungu mwema,
Kuacha yanaponza, na kukumbatia mema,
Muda sasa wa kuanza, ili tubaki salama,
Poteza ya duniani, uyapate ya mbinguni.

7:Dhambi zinazotusonga, kwa Mungu ni uhasama,
Vema sana kujipanga, mbele zisijesimama,
Kuamini mbele songa, Mungu mtoa uzima,
Poteza ya duniani, uyapate ya mbinguni.

8:Ruthu aliacha vyote, na kuvisukuma nyuma,
Na sisi kuacha vyote, kuwa na Mungu ni vyema,
Mwisho ni kupata vyote, hata milele uzima,
Poteza ya duniani, uyapate ya mbinguni.

9:Wewe kumpenda Mungu, hilo kweli jambo jema,
Hata uone uchungu, dunia iache nyuma,
Mungu kwako awe fungu, la maana tena jema,
Poteza ya duniani, uyapate ya mbinguni.

10:Ruthu aliacha vyote, hakuangalia nyuma,
Nawe sasa acha vyote, usiangalie nyuma,
Mema ya Mungu upate, ulinzi pia heshima,
Poteza ya duniani, uyapate ya mbinguni.
(Ruthu 1:8-18)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

@Moto Ulao Online Church

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news