Serikali na wizara tumepata pigo-Waziri Mavunde

DAR-Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameuelezea mchango mkubwa wa aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Wizara ya Madini,marehemu Edson Nkongo katika kuboresha na kuongeza makusanyo ya maduhuli ya Sekta ya Madini.
"Edson kwa kushirikiana na wenzake, alianzisha mifumo bora ukiwemo wa Masoko ya Madini, ambao umeleta mageuzi makubwa katika ukusanyaji wa maduhuli na kueleza kuwa umesaidia kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli kutoka shilingi bilioni 116 hadi kufikia shilingi bilioni 753 katika Mwaka wa Fedha 2023/24, na kuongeza mwaka huu tunatarajia kukusanya shilingi trilioni moja," amesema Waziri Mavunde.
Ameyasema hayo leo Machi 15, 2025 wakati akitoa salamu za rambirambi za Wizara kumuaga mtumishi huyo aliyefariki dunia Machi 12, 2025 katika Hospital ya Tumbi- Kibaha alipokuwa akipatiwa matibabu na kusema, Edson anabaki kuwa nguzo kuu kwenye mabadiliko ya Sekta ya Madini na kwamba utaalam wake umeisaidia nchi.

‘’Edson alikuwa mbunifu aliyejua anachopaswa kufanya, atabaki kwenye kumbukumbu zetu. Kupitia yeye na wenzake, amesaidia kuongeza mapato ya sekta kutokana na mifumo aliyoianzisha, hali ambayo ilifanya nchi nyingi kuja nchini kujifunza,’’ amesema Waziri Mavunde.
Ameongeza kwamba mbali ya mifumo inayotumiwa katika Sekta ya Madini, pia alihusika katika kamati za kitaifa kuandaa mifumo mingine ikiwemo mfumo wa Luku wa Tanesco na kuongeza, "Serikali na Wizara tumepata pigo,’’ amesema Waziri Mavunde.

Akisoma wasifu wa marehemu Edson kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini Augustine Olal amesema,marehemu Edson alifanya shughuli za mfano ikiwemo kuanzisha mfumo wa Local Content kwa kushirikiana na wenzake na kumweleza kuwa alikuwa mtumishi mwenye bidii ya kazi na mwadilifu.

Olal ametoa shukrani kwa familia ya marehemu, Hospital za Mlonganzila, Regency, Mloganzila na Tumbi Kibaha alikopatiwa matibabu.
Naye, Mchungaji Petro Lazaro aliyeongoza ibada ya mazishi akizungumza katika ibada hiyo amewataka waombolezaji kuishi maisha ya unyenyekevu na kuwatumikia wengine.

‘’Edson ameacha somo la maisha tunayopaswa kuishi kama watu tunaomtumaini Mungu, amefanyika baraka kwa watanzania kwa muda mfupi, hii ni kutokana na namna waombolezaji walivyomwelezea ikiwemo wasifu uliosomwa,’’ amesema mchungaji Lazaro.

International news

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post