DODOMA-Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameeleza ķuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imekuja mkakati maalum wa kuwawezesha Wachimbaji Wadogo kupiga hatua zaidi na kufaulu na hatimaye kumiliki migodi mikubwa kupitia mpango maalum utakaorahisisha upatikanaji wa mitaji, teknolojia ya kisasa, na kuwajengea uwezo endelevu wa uchimbaji na kibiashara.

Waziri Mavunde, amesema kuwa mpango huo utasaidia Wachimbaji Wadogo kupiga hatua na kuwa Wachimbaji wa Kati, hatimaye kuwa wamiliki wa migodi mikubwa inayochangia kikamilifu katika Pato la Taifa na uchumi kwaujumla.
Kuwatambua Wachimbaji
Mhe. Mavunde amewaelekeza watendaji wa Wizara kupitia Tume ya Madini kuandaa mfumo wa kutambua Wachimbaji Wadogo wanaofanya vizuri katika shughuli za uchimbaji ili waingie kwenye mpango maalum wa kuwawezesha kwa awamu hatimaye kupiga hatua na kuona manufaa ya uchimbaji wao.

“Sote tunafahamu mchango wa Wachimbaji Wadogo katika maduhuli ya Serikali, hivyo tunataka kuona wachimbaji wadogo wanakuwa wachimbaji wa kati na hatimaye kuwa wakubwa.
"Tunatengeneza mfumo wa kuwatambua wale wenye bidii, weledi, katika sekta ili kuwawezesha hadi kufikia hatua ya kumiliki migodi mikubwa, tunataka miaka michache ijayo kuwepo na mabilionea Wakitanzania waliotokana na Sekta hii,” amesema Waziri Mavunde.
Mfuko wa Dhamana
Waziri Mavunde amesema kuwa, ktika mkakati huo, Serikali kupitia Wizara ya Fedha, itatumia Mfuko wa Dhamana wa Serikali (Export Guarantee Scheme) ambao utatumika kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo nafuu ili wawezekuendesha shughuli zao ikiwemo kununua mitambo na vifaa vya kisasa vya uchimbaji na kwamba hatua hiyo inalenga kuwatoa Wachimbaji Wadogo kutoka katika uchimbaji wa majaribio na kuwapeleka katika uchimbaji wa kisasa wenye tija zaidi.
“Tunataka kuwapa wachimbaji wadogo uwezo wa kumiliki mitambo bora ili waongeze uzalishaji na kuongeza mapato yao.
"Kupitia mfuko wa dhamana, wachimbaji wataweza kupata mikopo yenye masharti nafuu ambayo itawawezesha kuwekeza zaidi kwenye sekta ya madini,” amesisitiza Waziri Mavunde.
STAMICO yapewa jukumu
Aidha, katika kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanapata taarifa sahihi za maeneo yenye madini kabla ya kuanza uchimbaji, Waziri Mavunde ameliagiza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambao ni walezi wa Wachimbaji Wadogo jukumu la kuongeza vifaa na mashine za uchorongaji (Rig Machine) na kuwa STAMICO inatakiwa kuhakikisha Wachimbaji Wadogo wanapata huduma za kisasa kwa gharama nafuu ili kuwawezesha kufanya uchimbaji wa kitaalamu na wenye ufanisi.
“Zile rig zikija hatutagawa kwanza mpaka tutakapoongeza na vifaa vya kisasa ili wachimbaji wadogo wasiwe wanachimba tu bali na kuweza kuchakata madini yao kwa wakati huohuo.
"Tunataka wachimbaji wapate huduma bora kwa gharama nafuu, na hii itaongeza uzalishaji wao kwa kiwango kikubwa,” ameongeza Waziri Mavunde.
Maandamano ya Pongezi
Katika hatua nyingine, Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini kupitia Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) wamepanga kufanya maandamano makubwa ya amani kwa lengo la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogo.

“Tumeona namna Serikali ya Mama Samia inavyowajali wachimbaji wadogo. Tumepewa mitaji nafuu, taratibu za leseni zimeboreshwa, na sasa tunapewa nafasi ya kumiliki migodi mikubwa. 

"Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, na tutafanya maandamano ya kumpongeza kwa kazi kubwa anayofanya katika sekta ya madini na kumuonyesha kuwa wachimbaji tunamuunga mkono,” amesema Bina.
Kwa juhudi hizi, wachimbaji wadogo wana matumaini makubwa ya kupiga hatua na kuwa sehemu muhimu ya wawekezaji wakubwa katika sekta ya madini nchini Tanzania. Serikali imeonyesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanapata fursa sawa na wawekezaji wakubwa, jambo linalotarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta hiyo na uchumi wa taifa kwa ujujumla.
Ushirikishaji
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amesema kuwa Serikali inajivunia mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo katika mnyororo mzima wa sekta ya madini, kwani wao ni wadau muhimu wanaochangia ukuaji wa sekta hiyo na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa sera, sheria, na taratibu zinazowekwa zinaakisi mahitaji halisi ya wadau wa Sekta ya Madini, wakiwemo wachimbaji wadogo, ili kuwezesha ukuaji endelevu wa sekta hiyo.