Serikali yakoleza kasi kuelekea uchumi wa kidijitali Zanzibar

ZANZIBAR-Katika jitihada zake za kukuza uchumi wa kidijitali nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti kwa kusaini makubaliano (MoU) ya ujenzi wa kituo cha kukuza ubunifu na Ujasiriamali wa TEHAMA Zanzibar utakaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 2.
Hafla ya utiaji saini ilifanyika mwishoni mwa wiki kati ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali uliozinduliwa Juni 2024.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, alisema ujenzi wa kituo hicho unaotarajiwa kuanza hivi karibuni ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mazingira ya ubunifu wa TEHAMA nchini, kuhakikisha kuwa wabunifu wa teknolojia wanapata nafasi ya kuendeleza mawazo yao na kuyageuza kuwa biashara zenye tija kwa taifa.
"Tunaelekea kwenye uchumi unaotegemea maarifa, na hivyo hatuwezi kupuuza umuhimu wa kuwekeza kwenye miundombinu ya ubunifu wa TEHAMA. Vituo hivi vitakuwa na vifaa na rasilimali zinazowawezesha wabunifu wetu, wajasiriamali wa TEHAMA, na vijana wanaoanzisha kampuni za teknolojia kupata nafasi ya kuendeleza miradi yao kwa ufanisi," alisema Dkt. Mwasaga.

Aliongeza kuwa, kituo cha Zanzibar ni sehemu ya mtandao wa vituo 10 vya kukuza ubunifu wa TEHAMA vinavyojengwa katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, ikiwemo Mwanza, Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Tanga, Lindi, na Zanzibar.

Lengo la vituo hivi ni kusaidia kuharakisha maendeleo ya sekta ya TEHAMA kwa kuwapatia vijana mazingira mazuri ya kujifunza, kubuni, na kuanzisha biashara zinazotumia TEHAMA.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohamed, amepongeza juhudi hizo na kusisitiza kuwa kituo hicho kitakuwa mhimili muhimu wa kukuza sekta ya TEHAMA Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

"Nchi yetu inahitaji mifumo thabiti ya ubunifu wa TEHAMA ili kuhakikisha kuwa vijana wetu wanakuwa sehemu ya mapinduzi ya kidijitali yanayoendelea duniani. Kituo hiki siyo tu kwamba kitawawezesha vijana wetu kubuni suluhisho za kidijitali, bali pia kitawasaidia kupata mafunzo, ushauri wa kitaalamu, na hata kufungua fursa za kimataifa," alisema Dkt. Khalid.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dkt. Habiba Hassan Omar, alisema serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa TEHAMA inakuwa sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu na wajasiriamali wa teknolojia.

Miongoni mwa malengo ya kituo hicho cha ubunifu wa TEHAMA Zanzibar ni pamoja na kuimarisha ubunifu katika sekta ya TEHAMA na kusaidia wabunifu wa teknolojia kuendeleza miradi yao, kujenga mnyororo wa thamani wa ubunifu wa TEHAMA, kutoa fursa za ajira na kuzalisha kampuni changa za TEHAMA, kuwezesha ushirikiano wa kimataifa kwa wabunifu wa TEHAMA na kusaidia ukuaji wa TEHAMA ili kuongeza mchango wake katika pato la taifa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Bi Hawwah Ibrahim Mbaye, alisema serikali itahakikisha kituo hicho kinakuwa na vifaa vya kisasa, mifumo ya kisasa ya mafunzo, na programu za kukuza ubunifu zitakazowawezesha vijana wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Hafla hiyo ya utiaji saini ilishuhudiwa na wadau mbalimbali wa sekta ya TEHAMA, maafisa wa serikali, na waandishi wa habari, ikiwa ni hatua muhimu katika kuelekea mapinduzi ya kidijitali nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news