Serikali yavuna shilingi Bilioni 3 ndani ya miezi 8

■Ni kupitia Sekta ya Madini Kagera,waita wawekezaji ndani na nje

KAGERA-Makusanyo ya maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini katika Mkoa wa Kagera yatokanayo na mrabaha, tozo na ada mbalimbali kwa mwaka wa fedha ulioanza Julai 2024/ 2025 ni Shilingi Bilioni 3.2.
Kagera ilipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 5.8 na mpaka mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu wa 2025 wamefanikiwa kukusanya kiasi hicho cha fedha kikiwa ni sawa na asilimia 82 ya lengo katika kipindi cha miezi nane.

Akizungumza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kagera, Nobert Mkopi amesema fedha hizo zimekusanywa kutokana na jitihada mbalimbali walizofanya katika usimamizi wa Sekta ya Madini katika halmashauri zote saba za Mkoa wa Kagera.
“Mkoa wa Kagera kwa maana Sekta ya Madini tunasimamia halmashauri zote saba kwa maana ya wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba, Biharamulo na Ngara, kuna shughuli mbalimbali za uchimbaji madini,”amesema Mkopi na kuongeza,

“Mkoa huu yanapatikana madini mbalimbali ikiwemo Bati, Dhahabu, Nickel, Wolframite (WO3), Madini ya Viwandani na Madini Ujenzi.
“Maeneo ya Kyerwa yanachimbwa madini ya bati, yanachimbwa kihalali kwa leseni za uchimbaji mdogo lakini pia kuna leseni kubwa ya utafiti na madini haya yanachangia asilimia 32 mpaka sasa ya maduhuli tuliyokusanya ya Shilingi Bilioni 3.2 na fedha nyingine zinatoka kwenye madini mengine ikiwemo dhahabu na ada mbalimbali za vibali na leseni," amesema Mkopi.

Aidha, amesema mwenendo wa ukusanyaji maduhuli sio mbaya na hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wana imani watafikia lengo lililokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Mkopi ametoa wito kwa wawekezaji kote nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini mkoani Kagera ambao una utajiri mkubwa wa madini mbalimbali ikiwemo Bati, Dhahabu, Nickel, Wolframite (WO3), Madini ya Viwandani na Madini ujenzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news