NA CHEDAIWE MSUYA
WF
KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza, Bw. Mohammed Kiande, amewataka wananchi kupanga matumizi yao vizuri, kuepuka madeni yasiyokuwa ya lazima, kujenga utajiri na kuongeza Uelewa wa Masuala ya kiuchumi.

Bw. Kiande alitoa rai hiyo wakati alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, Taasisi za Serikali na Binafsi ambayo ipo mkoani Mwanza kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali.
“Kupitia elimu hii, unaweza kuwekeza katika mipango ya muda mrefu kama vile akiba ya kustaafu na uwekezaji wa mali kupitia maarifa haya yatasaidia kutambua fursa na kuepukana na uwekezaji wa hatari au udanganyifu”, alisema Bw. Kiande.
Aliongeza kuwa Wananchi wajifunze jinsi ya kutengeneza bajeti inayolingana na kipato chao na kuweka akiba kwa ajili ya dharura na kufanya uwekezaji katika hisa, ardhi pamoja na biashara.
Bw. Kiande alifafanua kuwa elimu ya fedha siyo tu ni muhimu kwa kuimarisha maisha ya kifedha, bali pia kwa kujenga jamii yenye uelewa bora wa masuala ya kiuchumi.
“Ikiwa kila mtu atachukua jukumu la kujifunza na kutumia maarifa hayo, tunaweza kupunguza changamoto za kifedha na kuimarisha uchumi wetu kwa ujumla”. Alisema Bw. Kiande.
Nae mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bw. Mussa Gwandake, alitoa pongezi kwa Wizara ya Fedha kwa kuwaletea elimu ya fedha katika mkoa wa Mwanza kwani elimu hiyo itawasaidia katika kukuza uchumi wao.
“Mafunzo haya yametufunza mbinu bora za usimamizi wa rasilimali, uwekaji akiba, na kuepuka madeni yasiyo ya lazima, tunathamini juhudi zenu katika kuinua uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya kifedha. Asanteni kwa kujali ustawi wetu wa kiuchumi” alisema Bw. Gwandake.


Nae Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Bi Lilian Michael, aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwapatia elimu wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwani itasaidia kuwafumbua macho wananchi na kuepukana na migogoro ya familia inayojitokeza.
“Kabla ya kukopa, ni vyema familia ijadili madhumuni ya mkopo, masharti yake na athari zake kwa kila mwanakaya kwani itasaidia kupima iwapo kuna njia mbadala za kupata fedha badala ya kukopa,’’alisema Bi. Lilian.